Timu ya Yanga imetumia saa moja kufanya maandalizi yake ya mwisho kwa ajili ya mchezo wa kesho dhidi ya Geita Gold utakaopigwa saa 10:00 jioni katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Yanga ambayo ilifika jijini hapa jana usiku imefanya mazoezi yake leo CCM Kirumba kuanzia saa 10:00 jioni mpaka saa 11:00 jioni na kwenda kupumzika.
Msafara wa kikosi cha Yanga umefika katika uwanja huo kwa kutumia mabasi madogo (Coaster) mawili, moja likiwa limebeba viongozi wa benchi la ufundi na lingine likiwabeba wachezaji.
Baada ya kufika, timu hiyo ilianza kujifua kwa mazoezi mepesi ya kurejesha utimamu, kugawa uwanja nusu na kucheza kwa kupasiana pasi kisha wakahitimisha kwa zoezi la kupanga msitari mmoja kupasha misuli na kukimbia kwa haraka chini ya usimamizi wa kocha wa viungo.
Hata hivyo, timu hiyo imefanya maandalizi hayo chini ya ulinzi mkali wa jopo la usalama wa timu hiyo huku mashabiki mbalimbali waliofika kushuhudia mazoezi hayo wakigomewa kuingia uwanjani na kuzua kelele.