Kikosi cha Yanga kimefanya mazoezi ya mwisho jana jioni katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Geita Gold utakaochezwa leo.
Yanga ambayo imetua Mwanza jana alfajiri kwa ndege imefanya mazoezi hayo yaliyoongozwa na Kocha Nasreddine Nabi kuanzia saa 10:50 jioni huku mashabiki wakiruhusiwa kuingia uwanjani kutazama na kuibua shangwe kubwa kwani michezo kadhaa ambayo timu hiyo imecheza jijini hapa mashabiki wamekuwa wakipigwa 'stop'.
Msafara wa kikosi cha Yanga uliingia katika Uwanja wa CCM Kirumba saa 10:20 jioni kwa kutumia basi kubwa la Nyamse Express tofauti na ilivyozoeleka ambapo timu hiyo imekuwa ikitumia mabasi madogo ambapo baada ya kushuka kwenye gari wachezaji walifanya matizi mepesi ya kuuchezea mpira ikiwamo danadana ili kurejesha utimamu wa mwili.
Nyota watatu wanaohofiwa kukosekana kwenye mchezo wa leo, Fiston Mayele, Joyce Lomalisa na Djuma Shaban wamefanya mazoezi na wenzao ambapo Mayele alianza kwa mazoezi ya kukimbia taratibu kuzunguka uwanja kabla ya kuungana na wenzake.
Baada ya hapo, saa 10:50 jioni wachezaji wote wameitwa katikati ya uwanja na kutengeneza umbo la duara ambapo kocha Nasreddine Nabi amefanya nao mazungumzo akiwaeleza mambo mbalimbali mazungumzo hayo yakidumu kwa dakika 15 hadi saa 11:04 jioni wakaanza tizi la kukimbia taratibu kuzunguka uwanja wakiongozwa na kocha wa viungo.
Katika mazoezi hayo Nabi amesisitiza wachezaji kutengeneza mashambulizi kuanzia kwa mabeki kwenda kwa mawinga bila kupoteza muda ambapo amejaribu kombinesheni ya mawinga Jesus Moloko na Dickson Ambundo, ya Denis Nkane na Bernad Morrison huku Haritier Makambo na Mayele wakiitumika kwenye eneo la mwisho kwa nyakati tofauti ambapo mazoezi yamehitimishwa saa 12:05 jioni.
Akizungumzia maandalizi ya timu hiyo kuelekea mchezo wa leo, Afisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe amesema uhitaji wa pointi tatu kwenye mechi hiyo ni mkubwa kwani ushindi wa leo utawajengea hali ya kujiamini kuelekea mtanange wa Kombe la Shirikisho na Club Africaine.
"Mashabiki waje kwa wingi watazame mchezo na wawapongeze wachezaji wao na watengeneze muunganiko na timu yao, dakika ya 44 wainuke wapige makofi na kuonyesha mabango yao yenye jumbe mbalimbali za kuihamasisha timu na kuwapongeza nyota wao," amesema Kamwe.