Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yaizidi mbinu Simba

013012070593e6b3e3cc721a13d314a6 Yanga yaizidi mbinu Simba

Mon, 28 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TIMU ya Yanga jana imevunja mwiko, baada ya kuchomoza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo mkali wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro.

Ushindi huo unavunja mwiko baada ya Yanga kushindwa kuibuka na ushindi katika uwanja huo kwa misimu mitatu mfululizo, ambapo imefungwa mara mbili na kutoka sare mara moja, pia ni sawa na kuzidi mbinu Simba, kwani watani hao hao walitoka sare ya 1-1 na Mtibwa kwenye uwanja huo huo hivi karibuni katika mchezo wa ligi hiyo.

Bao lililowekwa kimiani na Lamine Moro dakika ya 60 akimalizia mpira wa kona uliochongwa na Carlos Fernandes ‘Carlinhos’, lililotosha kuwahakikishia Yanga kutoka na pointi tatu na kuvunja mwiko wa kushindwa kupata matokeo katika uwanja huo.

Carlinhos amezidi kujizolea sifa ndani ya kikosi cha Yanga kwa kucheza vizuri mipira iliyokufa, kwani hiyo ni mara yake ya pili baada ya kufanya hivyo dhidi ya Mbeya City, pale alipopiga kona na Moro kufunga kwa kichwa.

Jana mchezaji huyo raia wa Angola alipiga tena kona na kumkuta Moro aliyefunga kwa shuti katika dakika ya 61 na kuiwezesha timu hiyo kuondoka na pointi tatu na kufikisha jumla ya pointi 10 baada ya mechi nne sawa na Simba iliyo nafasi ya pili, lakini Yanga ikishika nafasi ya tatu kutokana na tofauti ya idadi ya mabao.

Mtibwa huo ni mchezo wake wa kwanza kupoteza, kwani tangu imeanza ligi imecheza mechi nne, imeshinda mchezo mmoja dhidi ya Ihefu FC, sare mbili mbele ya Simba na Ruvu Shooting na wapo katika nafasi ya tisa.

Mara baada ya mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, alisema kumuamzisha Carlinhos kwenye mchezo huo tofauti na mechi zilizopita ulikuwa mpango wa kuhakikisha wanaondoka na ushindi.

“Unajua watu wengi wamekariri Carlinhos sio mzuri sana kwenye viwanja kama hivi, lakini tulikuja na mpango wa kumuanzisha kwenye mchezo tofauti na michezo iliyopita kwa sababu anaweza kutoa kitu cha tofauti cha kuinufaisha timu na ndicho alichokifanya,” alisema Mwambusi.

Mchezo huo ulianza kwa ushindani mkali, ambapo kila upande ulionekana kudhamiria kutafuta ushindi, lakini hadi wanaenda mapumziko vikosi vyote vilionekana kutokuruhusu nyavu kutikiswa.

Mchezo mwingine wa ligi hiyo uliochezwa jana, Mwadui FC ilichomoza na ushindi wa kwanza wa mabao 2-0 dhidi ya Ihefu FC, baada ya kupoteza mechi tatu za mwanzo. Mchezo huo ulifanyika kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, mkoani Shinyanga, ambapo mabao ya Mwadui yaliwekwa kimiani na Fred Felix dakika ya sita na Wallace Kiango dakika ya 37.

Nayo Ruvu Shooting na Biashara United zilitoka suluhu katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Ligi hiyo itaendelea tena leo ambapo Coastal Union itaikaribisha JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.

Chanzo: habarileo.co.tz