Yanga bado ipo jijini Dar es Salaam ikijifua kujiandaa na mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh ya Sudan mchezo utakaopigwa Rwanda, lakini tayari vaibu la mashabiki wa timu hiyo limeteka jiji la Kigali litakalotumiwa kwa mchezo huo utakaochezwa Jumamosi.
Yanga watakuwa wageni wa Wasudani katika pambano litakalopigwa kwenye Uwanja wa Kigali Pele (zamani Nyamirambo), huku mashabiki wa soka jijini Kigali wakiwa na hamu kubwa ya kuiona timu hiyo na taarifa kwamba kuna mashabiki wengine watakaotoka jijini kwenda huko limewashtua maofisa wa Shirikisho la Soka la Rwanda (Ferwafa) ambao wameanza kujipanga mapema ili mambo yaende freshi katika mechi hiyo.
Sahau mashabiki kutoka Tanzania ambao hadi sasa ni zaidi ya mabasi 10, kutoka mikoa mbalimbali ikiwamo Dar es Salaam yameandaliwa kuwasafirisha hadi Nyamirambo, Rwanda kushuhudia mchezo huo, huko Kigali kwenyewe Wanyarwanda nao wamejipanga kuipokea Yanga kwa shangwe la kutosha.
Ofisa Habari wa Ferwafa, Julius Karangwa alithibitisha kuwapo kwa mashabiki wengi wanaoisubiri mechi hiyo na tayari maandalizi yameanza mapema ikiwamo suala la kuanza kuuzwa kwa tiketi kwa njia ya mtandao wiki ijayo kwa lengo la kutaka kuthibiti idadi ya mashabiki watakaotakiwa kuingia uwanjani.
Karangwa alisema kwa sasa Ferwafa imeweka nguvu zote kwa mechi ya timu ya taifa hilo dhidi ya Senegal, itakayopigwa Septemba 9, mwaka huu na baada ya hapo macho yote yatageuziwa kwa mechi ya Yanga na Merreikh.
“Kila kitu kinaendelea vizuri. Kwa sehemu kubwa maandalizi ya mchezo huu yanafanywa na uongozi wa Merrikh ambao ni wenyeji. Sisi Ferwafa tunatoa ushirikiano pale tunapohitajika,” alisema Karangwa na kuongeza;
“Kwa sasa tupo bize na timu ya taifa, lakini tukimaliza mechi yetu dhidi ya Senegal tutageukia mchezo huo na naamini kila kitu kitaenda vizuri kwa pande zote.”