Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yaitaka rekodi mpya kwa Medeama CAF

Yanga Caf Mks Yanga yaitaka rekodi mpya kwa Medeama CAF

Thu, 7 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika kuhakikisha anapata pointi tatu za kwanza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na dhidi ya Medeama SC, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, anatarajia kuwachanganya wapinzani wao hao, kwa kufanya mabadiliko madogo ya kikosi chake kuelekea mechi yao hiyo ya tatu kwenye hatua hiyo.

Yanga ambayo imeshacheza michezo miwili ya hatua hiyo ya makundi, ikianzia ugenini nchini Algeria ambapo ilipoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya CR Belouizdad kabla ya kurejea nyumbani katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Ahly ya Misri, Ijumaa itashuka katika Uwanja wa Baba Yara Sports (pia ukijulikana kama Uwanja wa Michezo wa Kumasi), kusaka alama tatu za kwanza.

Kama itapata ushindi, kwanza itaandika rekodi yao dhidi ya Medeama kwa kuifunga mara ya kwanza katika historia yake tena nyumbani, lakini huo utakuwa ushindi wao wa kwanza kwenye hatua hiyo msimu huu.

Mara ya kwanza timu hizo kukutana katika michuano hiyo ilikuwa mwaka 2016, Yanga ikikubali kichapo cha mabao 3-1 ugenini na mechi ya marudiano kutoka sare ya bao 1-1 hapa nchini.

Mabadiliko ambayo Gamondi anatarajia kuyafanya ni katika safu ya ulinzi baada ya beki Joyce Lomalisa kutoongozana na timu kutokana na kuwa majeruhi baada ya kuumia kwenye mchezo uliopita dhidi ya Al Ahly ya Misri na nafasi yake kuchukuliwa na Nickson Kibabage.

Tayari Kikosi cha Yanga kiliondoka tangu jana alfajiri kuelekea Ghana kwa ajili ya kusaka alama tatu muhimu zitakazoweza kuwatoa mkiani mwa Kundi D, lakini kutegemeana na matokeo ya mchezo kati ya Al Ahly dhidi ya Belouizdad.

Al Ahly inaongoza msimamo wa Kundi D ikiwa na pointi nne ikifuatiwa na Medeama na Belouizdad ambazo kila moja ina alama tatu huku Yanga ikiwa na moja, hivyo kama itashinda na miamba hiyo ya Misri kuwachapa Waalgeria hao, itapanda hadi nafasi ya pili.

Akizungumza na Nipashe jana, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, alisema wachezaji wote wako na morali kubwa kwenda kutafuta furaha za mashabiki wa Yanga na kufikia malengo yao.

Alisema katika kikosi hicho hatakuwapo Lomalisa ambaye yuko kwenye uchunguzi baada ya kuumia katika mechi iliyopita dhidi ya Al Ahly na nafasi yake kuchukuliwa na Kibabage .

“Ni kweli tutamkosa Lomalisa, lakini hatuna presha kutokuwapo kwake kwa sababu yupo Kibabage ni mzuri na atafanya kazi yake ipasavyo, tumeshamwona katika michezo iliyopita jinsi anavyocheza.

Presha ya mchezo ni lazima kwa sababu kila dakila 90 zinapokamilika basi mahesabu yanabadilika, mchezo ni mgumu tunaenda kucheza ugenini na ukizingatia Medeama wamemfunga aliyetufunga CR Belouizdad, hivyo watakuwa wanajiamini.

"Watambue tu kuwa Yanga si mpinzani mwepesi, tunahitaji kutafuta matokeo mazuri ikiwamo ushindi ili hesabu zetu ziweze kukamilika,” alisema Kamwe.

Aliongeza kuwa wanatambua katika rekodi dhidi ya Belouizdad walipoteza ugenini mabao 3-1 mwaka 2016 na katika mchezo wa marudiano kutoka sare ya bao 1-1 nyumbani, hivyo wanasahau hayo na wanaenda kutafuta ushindi ili kukamilisha hesabu zao.

“Tunajua historia lakini hesabu zetu ni jinsi ya kufikia malengo yetu, tumepoteza mechi moja, kutoka sare moja, sasa tunahitaji alama tatu za michezo iliyopo mbele yetu tukianza dhidi ya Medeama," alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: