Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yaishtukia US Monastir Dar

YANGA DUBAI 1 1140x640 Yanga yaishtukia US Monastir Dar

Thu, 16 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga wanajiwinda na mechi ya nyumbani ya Kundi D ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Monastir ya Tunisia Jumapili, lakini wameshtukia jambo na kuamua kuingia chimbo kuweka mambo sawa.

Mtaalamu mmoja wa timu hiyo amewahamishia gym ili kutafuta stamina na pumzi za kutosha kuwakabili wapinzani wao na fasta zoezi likatekelezwa.

Kocha wa viungo wa timu hiyo, Helmy Gueldich ‘Manywele’ ndiye aliyeshtukia jambo hilo baada ya kutonywa na msoma mchezo mpya wa timu hiyo, Khalil Ben Youssef, kwamba lazima kifanyike kitu naye (Helmy) kuamua kuongeza dozi. Ipo hivi.

Yanga juzi ilikuwa katikati ya jiji la Dar es Salaam ikitumia saa tatu kujiweka sawasawa eneo hilo ikiwa chini ya Helmy anayewaimarisha mastaa wa timu hiyo zaidi msimu huu.

Hiyo ilikuwa ni ratiba pekee ya siku hiyo ambapo dozi hiyo iliwalazimu makocha wao kuwahurumia wachezaji hao na kuwaambia zoezi hilo ndio kitu pekee ambacho wangefanya na baada ya hapo wakatakiwa kwenda kupumzika.

Jana sasa kazi ikabadilika wakirejea uwanja wa mpira kwa mazoezi mengine ya kuimarisha zaidi miili ya wachezaji wao huku ufundi ukiwa kidogo ambapo tayari kikosi hicho kimeshaingia kambini kujiwinda na mchezo huo.

Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi ameliambia Mwanaspoti kuwa kuna umakini mkubwa katika wiki yao hii ya mazoezi lengo likiwa kuingia na ukamilifu katika mchezo dhidi ya Monastir ambao ameupa jina la fainali ndogo. Nabi alisema watakuwa na wiki ngumu kuhakikisha wanapambana na Monastir ambao ndio vinara wa kundi D huku akifurahia morali nzuri ya wachezaji.

“Hii ni wiki ambayo tunatakiwa kumaliza kila changamoto yetu ya makosa tunayofanya kabla ya siku ya mchezo, tutakuwa na ratiba ngumu ya kuhakikisha kila kitu tunakiweka sawa,” alisema Nabi na kuongeza;

“Hii ni mechi ya fainali kwetu, tunakwenda kucheza mechi ngumu nyingine ya kundi letu, jambo zuri ni kwamba wachezaji wanajua kuwa wana deni la kujisahihisha kufuatia makosa ya mchezo wa kwanza wakijua sasa watacheza nyumbani mbele ya mashabiki wao ambao wamekuwa na heshima kubwa ya kuwafuata kokote wanakokwenda.”

Wakati Yanga ikianza maandalizi hayo Mwanaspoti linafahamu kuwa kuna taarifa zaidi za ubora wa Monastir, zimetua na mtaalam wao mpya wa kuchambua mikanda ya wapinzani Khalil Ben Youssef.

Ben Youssef ambaye ameongezwa kwenye benchi la Yanga ameshawapa makocha wa timu hiyo makosa ambayo Monastir wanayafanya katika mechi zao, pia ametoa makosa makubwa ambayo Yanga iliyafanya katika mchezo wa kwanza. Katika mchezo huo wa awali, Yanga ililala mabao 2-0 yaliyofungwa katika dakika 15 za kwanza na Yanga kupoteza ugenini.

Monastir imeshatangulia robo fainali kwa kufikisha pointi 10, huku Yanga ikiwa ya pili na pointi saba, ikifuatiwa na TP Mazembe yenye pointi tatu na Real Bamako ikiwa mkiani na pointi mbili baada ya mechi nne.

Chanzo: Mwanaspoti