Klabu ya Yanga, jana Oktoba 16, 2023, imelipongeza Shirika la Bima la Taifa (NIC) baada ya kutimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake.
NIC Insurance ni mdhamini rasmi wa Yanga SC kwenye Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi ambapo hivi karibuni mkataba baina ya pande hizo mbili ulisainiwa ambapo NIC watatoa kiasi cha shilingi milioni 900 ndani ya kipindi cha miaka mitatu.
Akizipokea pongezi hizo, Elirehema Doriye ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji NIC, alisema:
“Nawashukuru sana ndugu zetu wa Yanga SC kwa kuungana nasi kwenye siku hii ya kutimiza miaka 60 ya Taasisi yetu. Ni matajarajio yetu tutaendelea kuwa bega kwa bega. Nimepokea salamu za Rais wa Yanga SC Eng Hersi Said. Nimuhakikishie tunajivunia sana uwepo wao kwetu.
“Tumeingia mkataba wa udhamini wa Yanga SC, hivyo kwenye mipango na mikakati yetu tutashirikiana nao kwa kiasi kikubwa. Tunatambua kuwa hawa ndio washirika wetu wakubwa, hivyo tutashiriki hata kwenye baadhi ya mikakati yao pia ili kuhakikisha tunasonga mbele.”
Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa Yanga SC, Andre Mtine, alisema: “Tunawashukuru sana NIC kwa kutushirikisha kwenye hafla yao ya kutimizia miaka 60. Sisi kama klabu tunatambua kuwa NIC ni chapa namba moja, tunathamini sana mchango wao kwetu na kwa jamii wanayoihudumia.
Ni heshima kubwa sana kufanya kazi na kampuni kubwa kama hii. Kwa upande wetu nasi tunafahamu kuwa NIC wanajivunia kufanya kazi na sisi. Kwa pamoja tutapiga hatua kubwa.”