Michezo Ligi kuu soka Tanzania Bara ikiwa ipo raundi ya 25 na imesalia michezo 5 kabla ya kumalizika kwa msimu, takwimu zinaonyesha Klabu ya Yanga inaongoza kwa kuchukua alama nyingi kwenye viwanja vyote nyumbani na ugenini licha ya kuwa imecheza michezo 24 kwenye Ligi msimu huu 2022-23.
Timu ya wananchi imekusanya jumla ya alama 65 kwenye michezo 24 waliyocheza mpaka sasa kwa ujumla nyumbani na ugenini.
Lakini alama 35 kati ya hizo 65 wamezipata katika uwanja wao wa nyumbani kwa kushinda michezo 11 na kutoka sare michezo 2 katika michezo 13 waliyocheza nyumbani ikiwa ndiyo timu iliyoshinda alama nyingi zaidi uwanja wa nyumbani wakifuatiwa na Azam FC waliokusanya alama 31 kwenye michezo 12 na Simba alama 29 kwenye michezo 11.
Kwenye viwanja vya ugenini Yanga bado ni vinara, wamekusanya alama 30 kwenye michezo 11 wameshinda michezo 10 na wamefungwa mchezo mmoja tu. Simba wanashika nafasi ya pili wameshinda alama 28 ugenini kwenye michezo 13 Sinda Big Stars wanashika nafasi ya 3 wamekusanya alama 19 kwenye michzo 13.