Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yageukia ngumi

Yanga Kamweeeee Yanga yageukia ngumi

Wed, 19 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Uongozi wa Klabu ya Yanga umeahidi kutia mkono pambano la 'Dar Boxing Derby' litakalofanyika Juni 29, mwaka huu katika viwanja vya Posta vilivyopo Kijitonyama, Dar es Salaam, kwa kuwa miongoni mwa wadhamini.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, Ofisa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ally Kamwe, alisema mchezo wa ngumi kwa sasa unapiga hatua kutokana na mabondia wa Tanzania kufanya vizuri katika mapambano yao.

Alisema 'Dar Boxing Derby' ni pambano lililojaa ubunifu mkubwa kwani mabondia ambao watacheza siku hiyo ni wale wenye viwango vikubwa.

"Yanga tumethibitisha tutadhamini pambano hilo kwa sababu tunajua kuna vipaji vingi vitaonekana siku hiyo, pia tutachagua mabondia ambao wana mapenzi na klabu yetu tutawasajili kwa lengo la kufufua ngumi kwenye klabu yetu," alisema Kamwe.

Kamwe alisema kama klabu watatoa zawadi kwa mabondia ambao watafanya vizuri, ikiwamo pambano kuu kati ya Nassib Ramadhan na Juma Choki.

Naye, promota wa pambano hilo, Meja Selemani Semunyu, ameziomba klabu nyingine ziwekeze katika ngumi kwa sababu mchezo huo una vijana wengi wenye vipaji.

"Ni faraja kuona klabu kubwa kama Yanga imekubali kudhamini ngumi kwa sababu wameona vipaji mbalimbali ambavyo vinatoka katika mchezo huu, milango ipo wazi kwa klabu zingine kuja kuunga mkono," alisema Semunyu.

Semunyu alisema mbali ya pambano la Nassib Ramadhan na Juma Choki, mabondia wengine watakaopanda ulingoni ni Tonny Rashidi ambaye atacheza na Oscar Richard, wakati Said Bwanga atapigana na Said Mkola, huku Haidari Mchanjo akitoana jasho na Charles Tondo, wakati pia akina dada Najma Isike akivaana na Nasra Msami.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live