Meneja wa Kikosi cha Young Africans SC, Walter Harrson, amezungumzia kinachoendelea kambini wakati huu wa mapumziko ya kupisha michezo ya Kalenda ya FIFA ambapo timu hiyo ipo katika maandalizi ya kuelekea michezo ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Machi 30, mwaka huu, kikosi hicho kitakuwa mwenyeji wa Mamelodi Sundowns katika mchezo wa kwanza wa robo fainali utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, kisha kwenda Afrika Kusini kurudiana, Aprili 5, 2024.
“Tupo katika wiki ya FIFA mwezi huu wa tatu, takribani wachezaji tisa wameitwa kwenye timu za taifa, hivyo kwa kiasi kikubwa sehemu ya kikosi haipo, lakini hawa ambao hawajapata nafasi ya kuitwa kwenye timu za taifa wamebaki hapa wanaendelea kupikwa.
“Kikubwa kocha anajiandaa kuipika timu ili kuweza kuwa katika hali nzuri ya kiushindani kuelekea mchezo unaofuata wa Champions League dhidi ya Mamelodi, lakini pia michezo mingine itakayofuata baada ya hapo,” alisema Harrson.
Kuhusu wachezaji walioitwa Taifa Stars ambao Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema litawaruhusu kuwahi kurudi kambini kutokana na kupewa nafasi ya kucheza mechi moja pekee badala ya mbili, Meneja amezungumzia hilo kwa kusema: “Kwa kweli ni habari nzuri.
“Kwa kipekee ni kuwashukuru TFF kwa kuweza kusikiliza kile ambacho sisi tulikiomba kama klabu kutokana na uzito wa mchezo ambao upo mbele na upatikanaji wa wachezaji husika na umbali wa sehemu waliyokwenda kucheza michezo ya Kalenda ya FIFA.
“Baada ya maombi yetu, wameweza kuyafanyia kazi na wamewasiliana na sisi tuhakikishe siku ambayo wachezaji watarudi baada ya kucheza mchezo wa kwanza dhidi ya Bulgaria.
“Hili kwetu ni jambo kubwa na litakuja kuongeza chachu kwenye kikosi, litakuja kutuongezea upana wa kikosi na kutengeneza mipango ya pamoja kuelekea kwenye mchezo unaofuata.”
NENO LAKE KWA MASHABIKI
“Moja ya kitu ambacho nimekishuhudia ni sapoti kubwa ambayo tumekuwa tukiipata kutoka kwa Wananchi, mashabiki wetu, imekuwa ya tofauti sana msimu huu.
“Hata juzi baada ya kupoteza mchezo hakukuwa na mrejesho mbaya kwa timu baada ya kile kilichotokea, na sisi tulikwenda kuwashukuru na kuwaomba radhi, inatokea kwenye mchezo.
“Wamekuwa na sapoti kubwa sana kwetu, kwa hiyo kama maandalizi haya yameanza kwa upande wetu, naamini mashabiki wataona jinsi gani wanapaswa kujiandaa kwa sababu ni michezo muhimu ambayo tunakwenda kushiriki inayokwenda kuwa na hatma na historia kubwa sana kwenye timu yetu.
“Hivyo kwa wale waliopo Dar es Salaam, nadhani kwao inaweza kuwa rahisi kununua tiketi baada ya utaratibu kutangazwa, lakini kuna wengine ambao wapo mikoani, ninaamini watakuwa na nafasi nzuri kwao kuja kushiriki nasi katika michezo hii ya kihistoria kwa maana ya kuja Dar es Salaam na wale wenye uwezo wa kwenda Afrika Kusini wataangalia namna ya kufanya kwa jili ya kuendelea kutupa nguvu zaidi na mwisho wa siku tuweze kutengeneza historia kwa pamoja,” alisema Harrson.