Ofisa Habari wa Klabu ya yanga, Ally Kamwe amefafdanua kuhusu Tamasha la Siku ya Wananchi ambapo mashabiki wa klabu hiyo waliojitokeza walishindwa kuujaza uwanja wa mkapa huku chanzo kikidaiwa kuwa ni kiingilio kuwa kikubwa.
Kamwe akihojiwa, amesema; “Tunamshukuru Mungu tamasha limemalizika salama, mashabiki, wananchama na Watanzania waliofuika kwenye Uwanja wa Mkapa wali-enjoy kwa asilimia kubwa ya kile ambacho walikitarajia, siwezi kusema ni asilimia 100 japo 90 kwa sababu kazi ya binadamu haziwezi kukosa kasoro.
“Nimeona mjadala wa mashabiki wa Yanga, waandishi na wachambuzi wakisema kiingilio kilikuwa kikubwa hivyo kikawa kikwazo kwa mashabiki kuhudhuria. Wanasema kwa vile lilikuwa ni tamasha basi ilitakiwa kiingilio kiwe rafiki ili kuruhusu mashabiki wengi kujaa uwanjani.
“Sisi kama viongozi hatujadharau kwa asilimia 100, tumepitia maoni na pale tulipoona kuna hoja tumechukua lakini yale ambayo hayana mashiko tumeachana nayo.
“Watu wanatakiwa wajue kwamba thamani ya klabu yetu imepanda sana kwa hii misimu mitatu ya hivi karibuni. Hata kama ukitaka kuiweka sokoni Yanga sasa hivi utapata mabilioni ya fedha.
“Thamani hii imekuja baada ya uongozi kutengeza benchi bora la ufundi, kusajili wachezaji wenye ubora na kufanya vizuri ndani na nje ya nchi. Mwaka jana tumecheza fainali ya CAF, si jambo dogo, tumetetea mataji yetu yote matatu ya ndani si kitu cha kawaida.
“Klabu inayopanda thamani lazima standard yetu ipande mara mbili. Lazima tusajili wachezaji wazuri, mchezaji kama Max (Nzegeli) huwezi kumpata kwa Tsh 2,000, lazima upambane kumshawishi ili umpate sokoni aje kwako.
“Kennedy Musonda tuligombea na TP Mazembe lakini akachagua kuja Yanga akiwa top scorer wa ligi ya Zambia katikakati ya msimu.
“Wanachama tuliwaambia bajeti yetu msimu ujao ni Tsh bilioni 20 na makusanyo yetu msimu uliopita tuliwaambia ni Tsh bilioni 2, kwa hiyo hii pesa ya bajeti haichimbwi kama viazi, wala kushuka juu kama mvua bali inapatikana kutokana na vyanzo rasmi vya mapato vya klabu ambapo miongoni mwake ni viingilio.
“Hii ni mbali na sponsors, kuuza bidhaa za klabu kama jezi, digital platforms za klabu pia zinaingiza pesa, lakini viingilio ni chanzo kikubwa cha mapato cha klabu, kwa hiyo mashabiki wanatakiwa wajue huu ni wajibu wao.
“Tamasha kama lile kuliandaa sio kazi rahisi, kuchukua timu kama Kaizer Chiefs, wanakuja watu zaidi ya 50, wasanii wazuri kwa ajili ya kutumbuiza. Lakini ikumbukwe kuwa msimu uliopita kiingilio kilikuwa ni hiki hiki Tsh 10,000 kwa mzunguko.
“Muitikio ni mkubwa japo hatukujaza uwanja, sababu za kutokuujaza uwanja haziuziani na kabisa na suala ya viingilio; Cha kwanza kilikuwa ni ratiba tuliyokuwa nayo mwanzoni ambayo ilituonyesha Julai 28 mpaka 30, kulikuwa na mechi za kwanza za CHAN Qualifier, na Agosti 4 mpaka 6 ilikuwa mechi za marudiano, Yanga tunatoa zaidi ya wachezaji watano kwenye timu ya Taifa.
“Kingine kuupata uwanja wa Taifa ambao ulikuwa umefungiwa haikuwa kazi nyepesi, tarehe pekee tuliyopangiwa ni Julai 22, vinginevyo tusingefanya kabisa tamasha hili na mashabiki wasingetuelewa.
“Tumetoka kuzindua jezi kwa Tsh 40,000, tumetangaza Wiki ya Mwananchi na kuanza promo ambayo ni wiki moja tu wakati zamani ilikuwa mwezi mzima. Wakati tunafanya promo tayari tunatangaza usajili wa wachezaji, hivi ndio vitu vimesababisha.
“Lazima mashabiki waelewe kuwa thamani ya klabu yao imepanda, mashabiki waliokuja wameiheshimisha sana klabu yao na mashabiki, niwaombe mashabiki wanalo jukumu la kupanda na thamani ya klabu yao ili waende nayo pamoja,” amesema Kamwe.