Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yaepuka janjajanja Algeria

Yanga Janja Janja.jpeg Yanga yaepuka janjajanja Algeria

Mon, 20 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mabosi wa Yanga wameonyesha wazi wanataka kuhakikisha wanapata pointi tatu katika mchezo wao wa makundi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya CR Belouizdad baada ya kumsafirisha mtu kwenda nchini Algeria kuweka mazingira sawa ili timu hiyo itakapofika ikute kila kitu kimekaa sawa na kujua namna ambavyo wapinzani wao wanavyotengeneza presha kabla ya mchezo huo.

CR Belouizdad itakaribisha Yanga Novemba 24 mchezo utakaochezwa katika uwanja wa Stade du 5 Juillet saa 4:00 usiku.

Mwananchi lilipenyezewa kwamba Mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh jana alfajiri alianza safari ya kwenda nchini Algeria kwa ajili ya kuweka mazingira sawa.

"Huyo anaenda kwa ajili ya kuhakikisha timu inapofika basi hakutokuwa na sintofahamu yoyote ile kuanzia usafiri, uwanja wa mazoezi na hata sehemu ya kufikia,"kilisema chanzo hicho.

Awali Hafidh alikuwa meneja wa timu hiyo lakini kwa sasa nafasi hiyo yupo Walter Harrison.

Wakati kigogo huyo akiwa ameondoka, kundi la kwanza la wachezaji wa Yanga ambao wapo kambini (Avic Town) wakiendelea na mazoezi wanatarajia kuondoka nchini kesho Jumanne.

Wakati mastaa waliopo Avic wakitarajia kuondoka kesho, wale waliopo Stars wenyewe wataanza safari Jumatano huku wale waliopo nje ya nchi wenyewe wataungana na timu huko huko Algeria wakitokea nchini mwao.

Benchi la ufundi la Yanga limepania kwani hayo yote yakifanyika hakuna mchezaji ambaye ataachwa haachwi mtu Yanga wanampango wa kuondoka na wachezaji wao wote bila kujali nani anacheza wakihofia uchovu wa baadhi ya mastaa waliotoka kutumika kwenye timu zao za taifa huenda wakashindwa kumaliza dakika 90.

Nyota wa kigeni ambao wapo nje ya timu na wataungana na wenzao juu kwa juu ni Dijgui Diarra, Khalid Aucho na Stephane Aziz Ki wakati wachezaji wa ndani ni Abutwalib Mshery, Dickson Job, Mudathir Yahya, Ibrahim Bacca na Nickson Kibabage.

Wakati huo huo Nahodha wa timu hiyo ambaye yupo kwenye majukumu ya timu ya Taifa Tanzania, Bakari Mwamnyeto alisema licha ya kwamba kwa sasa hayupo kwenye klabu yake anatambua wana mchezo mgumu.

Mwamnyeto alisema licha ya ugumu wa ratiba uliopo unawafanya wachezaje kwa maelekezo na akili zaidi kwani wanatambua umuhimu wa nafasi zao stars na Yanga huku akikiri kuwa wamesisitizwa kujilinda ili kuwa katika wakati mzuri wa kulitumikia taifa na Yanga.

“Unajua ukuta wa Yanga ndio ukuta wa Stars tupo hapa kuipambania nchi na bado tutahitajika kwenda kuendelea tulipoishia kwa kujihakikisha timu inaanza vyema mchezo wake wa kwanza kwenye kundi D;

“Kocha Miguel Gamondi kaniambia mimi nikiwa kama nahodha natakiwa kuwaongoza wenzangu ambao nacheza nao pamoja Dickson Job, Mudathir Yahya, Ibrahim Abdallah ‘Bacca’ kuhakikisha tunakuwa makini zaidi tusipate shida Yanga na Stars zinatutegemea.” alisema.

Mwamnyeto alisema hawatakuwa na muda wa kupumzika wakimaliza mechi wataunga moja kwa moja uwanja wa ndege tayari kwaajili ya kwenda kuungana na kikosi cha Yanga kwaajili ya mchezo huo dhidi ya CR Belouizdad Novemba 24.

“Tunashukuru Mungu tumeanza na ushindi ugenini hii imetupa nguvu tuna mchezo mwingine nyumbani matokeo mazuri tutakayopata yataongeza morali kwetu safari haitakuwa ngumu tutaondoka na nguvu ya kwenda kupambana zaidi.” alisema Mwamnyeto.

Yanga imepangwa kundi D na timu za CR Belouizdad, Al Ahly ya Misri na Medeama ya Ghana.

Chanzo: Mwanaspoti