Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yaeleza sababu vijana benchi la ufundi

E437bd5f0a0524285b5e9ae9ef651255 Yanga yaeleza sababu vijana benchi la ufundi

Wed, 3 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

UONGOZI wa Yanga umesema umeamua kuwaongeza vijana kwenye benchi la ufundi ili kwenda na kasi ya soka la kisasa.

Juzi Yanga ilimtambulisha Nizar Khalifan kuwa kocha msaidizi kuchukua nafasi ya Juma Mwambusi ambaye aliomba kupumzika kutokana na matatizo ya kiafya, pamoja na Edem Mortotsi kuwa kocha wa viungo.

Mshauri Mkuu wa klabu hiyo kuelekea kwenye mfumo wa mabadiliko, Senzo Mbatha alisema wameamua kuwaongeza vijana kwenye benchi lao la ufundi ili kwenda na kasi ya soka la kisasa.

“Tunahitaji kuongeza thamani ya ubora katika benchi ndio maana wote ni vijana na hata kocha mkuu wetu ni kijana ili kuendana na soka la kisasa.”

“Ninaona watu ambao wamechaguliwa ni watu wazuri hivyo ni suala la kusubiri na kuona namna ambavyo tutaendelea kupambana,” alisema Senzo.

Yanga inaongoza Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 44 baada ya kucheza michezo 18.

Wakati huo huo, Ofisa Habari wa timu hiyo, Hassan Bumbuli amefungiwa kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha miaka mitatu kwa kutotii uamuzi wa Kamati ya Maadili dhidi yake.

Bumbuli alishtakiwa kwa kutotii uamuzi wa Kamati ya Maadili uliokuwa umetolewa dhidi yake Septemba 28, mwaka jana na kutakiwa kulipa faini ya Sh milioni 5 na kutofanya kosa la kimaadili kwa kipindi cha miaka miwili uamuzi ambao hakuutekeleza wala kuukatia rufani.

Mwingine aliyefungiwa na kamati hiyo ni Katibu Mkuu wa Lipuli FC, Julius Leo kwa miaka mitatu na faini ya Sh milioni 3 kwa kosa la kutoa taarifa za uongo kuhusu kiasi ambacho Lipuli ilikuwa inaidai TFF ikiwa ni zawadi ya mshindi wa pili wa Kombe la Shirikisho na kukosa umakini wa kutunza nyaraka na siri za ofisi.

Pia kamati hiyo haikuwakuta na hatia Kaimu Mwenyekiti wa Lipuli FC Ayoub Kihwelo na Mwenyekiti wa Chama cha Soka Wilaya ya Kibaha (Kibafa) Pwani, Robert Munisi.

Chanzo: habarileo.co.tz