Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yadaiwa kuingilia kati dili la Awesu

Awesu X Yanga Simba Yanga yadaiwa kuingilia kati dili la Awesu

Thu, 15 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati sakata likiwa halijapoa la kiungo Awesu Awesu kugoma kurejea katika klabu yake ya KMC kutokana na usajili wake kwenda Simba kuonekana ni batili, Yanga ni kama imepigilia msumari, baada ya kutajwa kuingilia dili hilo.

Ipo hivi: Awesu Awesu alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja na KMC, akaandika barua ya kuvunja na kuilipa timu hiyo Sh50 milioni na kujiunga na Simba ambako amesaini mkataba wa miaka miwili, hata hivyo ikagundulika kakiuka baadhi ya vipengele, hivyo uongozi wa timu hiyo, ulikwenda kushitaki katika Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka nchini (TFF).

Katika kesi hiyo, KMC ikaonekana ina haki ya kuendelea kubaki na mchezaji wao, ikatangaza ofa kwa Simba endapo ikimhitaji itatakiwa kupeleka Sh200 milioni ili kuununua mkataba wake, huku kamati hiyo ya TFF ikiwaonya Wekundu wa Msimbazi na kuwataka wafuate taratibu sahihi za kusajili wachezaji.

Licha ya uongozi wa KMC kushinda kesi hiyo, Awesu Awesu aliendelea na mgomo wa kutorejea kikosini na imeelezwa asubuhi ya leo Agosti 15, amefanya mazoezi na Simba.

Wakati hayo yakiendelea, huku KMC ikitoa siku tatu kwa mchezaji tangu jana Jumatano, kwamba asiporejea itamchukulia hatua, Yanga imetia timu na kupeleka ofa ya kibunda cha maana.

Imeelezwa Yanga imepeleka Sh150 milioni taslimu, ili kutaka saini ya Awesu Awesu awe sehemu ya kikosi chao msimu ujao.

Taarifa kutoka kwa mmoja wa viongozi wa KMC, zinasema: "Hadi muda huu, kikao kinaendelea baina ya uongozi wa KMC na Yanga ili kumaliza biashara ya mchezaji huyo, hivyo lolote linaweza likatokea."

Chanzo: Mwanaspoti