Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yachorewa ramani nzima Tunisia

Yanga Ramani Yanga yachorewa ramani nzima Tunisia

Fri, 4 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati siku tano zijazo Yanga itakuwa mjini Tunis, Tunisia kuikabiri Club Africain katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika, timu hiyo imepewa mbinu za kuifunga miamba hiyo.

Yanga inahitaji ushindi au sare ya mabao itakaporudiana na Club Africain, Novemba 9, ili kutinga hatua ya makundi kwenye mashindano hayo baada ya juzi kulazimishwa suluhu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Hata hivyo, timu hiyo imeambiwa kama ikitulia ina uwezo wa kuwashangaza Watunisia hao ambao wanatajwa kuwa na fujo na fitina za soka wakicheza nyumbani, ingawa pia inatajwa kupata upinzani kwa baadhi ya mashabiki ikiwa kwao.

“Kama Yanga itajipanga vizuri itaifunga, waache kuzifikiria fitina na fujo za wapinzani, wao wapambane uwanjani kutafuta matokeo tu,” alisema nyota wa Kipanga, Abdillah Suleiman Kombo ‘Mido Kubwa’ aliyekuwa miongoni mwa wachezaji waliofungwa na timu hiyo nchini Tunisia.

Alisema ukiachana na matokeo ya karibuni ya kimataifa, timu hiyo si tishio sana kwenye ligi yao, huku akifichua kwamba Yanga inachotakiwa ni kuidhibiti dakika 30 za kipindi cha kwanza na ikiweza itangulie kufunga lakini wakianza kufungwa basi timu hiyo itacheza hadi na waokota mipira.

“Wakiwa wanaongoza, hata waokota mipira wanajichelewesha kuwapa mipira, pia mashabiki wao wana fujo hadi za kurusha chupa uwanjani, lakini Yanga wala wasizingatie, ingawa kwenye usalama askari wao wako vizuri.

“Vyumba vya kubadilishia nguo pia hakuna shida na hata hotelini, kuna ulinzi, sisi tulipokwenda askari wao walikuwa wengi na walitulinda kuhakikisha hatupati tatizo kuanzia hotelini hadi tunaingia uwanjani,” alisema Mido Kubwa.

Akiwazungumzia ndani ya uwanja, kiungo huyo alisema wana uwezo wa kuuchezea mpira na ukiwa kwa wapinzani wanahakikisha wanakukabia golini kwenu hawakupi nafasi.

“Hiyo ndiyo faida yao, hawapendi wapinzani wacheze wakiwa kwao na wana uwezo wa kufunga kwa kaunta sana, kama Yanga ikijiamini na kushambulia kwa kushitukiza itapata matokeo.

“Sisi walitufunga kwa mabao mengi ya ‘kaunta’, ingawa pia mabao yao wanayafunga kwa kutokea pembeni, wana kasi kubwa hasa dakika 30 za kwanza, baada ya hapo wanaanza kupunguza na kuchoka, Yanga ikiwafunga ndani ya muda huo watawavuruga,” alisema.

Kocha wa Kipanga, Hassan Kitimbe alisema kama Yanga itawamudu na kuwabana kipindi cha kwanza na kufunga bao la mapema, nafasi ya kusonga ipo.

Chanzo: Mwanaspoti