Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yaanza kunoga!

Yangaz Pic Data Yanga yaanza kunoga!

Sat, 20 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

TAIFA lipo kwenye msiba mzito wa kuondokewa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mmoja ya wanamichezo namba moja, John Magufuli, lakini unaambiwa huko Jangwani mambo ni moto na waliokuwa wakiibeza Yanga wajiandae kufanyiwa sapraizi.

Ndio, kwa jinsi Yanga inavyopiga tizi ikiwa chini ya Kocha Juma Mwambusi na namna wachezaji walivyo na morali kubwa kwa sasa ni wazi, mashabiki wa klabu hiyo wajiandae tu kutabasamu pale kikosi chao kitakaposhuka uwanjani baada ya maombolezo ya siku 14 zilizotangazwa na serikali.

Nani hajui namna kocha Mwambuzi alivyo mtaalamu wa kutengeneza ufiti na pumzi kwa wachezaji, si mnaikumbuka ile Mbeya City ya msimu wa kwanza ilivyokuwa? Sasa unaambiwa tizi linalopigwa chini yake kwa sasa kwenye mazoezi ya timu hiyo Avic Town, Kigamboni sio mchezo na limefanya wachezaji wachangamke kinoma na kila mmoja kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Gazeti lako makini Mwanaspoti lilipiga kambi, kwenye mazoezi hayo ya Yanga yanayofanyika Kigamboni na kushuhudia vijana wa Jangwani wakipigishwa tizi la nguvu, huku ikionekana wazi mastaa wa timu hiyo wamejazwa upepo ambao kama wapinzani wasipojipanga lazima waumie.

MORALI YA JUU

Siku chache zilizopita mashabiki wa Yanga walikuwa wanyonge baada ya kushuhudia timu yao ikidondosha pointi 11 kati ya 18 ilizokuwa ikiziwinda katika mechi zao sita za raundi ya pili, hasa baada ya kufumuliwa 2-1 na Coastal Union jijini Tanga na kupata sare na Polisi Tanzania.

Mechi hizo ndizo zilizomtemesha kibarua kocha Cedric Kaze na nafasi yake kupewa Mwambusi, huku ikionekana hata wachezaji wa Yanga wakipigwa ganzi na matokeo hayo yaliyowasononesha mashabiki wao, lakini sasa kwenye tizi linaloendelea Kigamboni, nyota wa timu hiyo wana mzuka.

Mastaa hao wanajituma kwa bidii huku wakionekana wakiwa na mzuka wa kupambana wenyewe kwa wenyewe na kuhamasishana sambambna na kuelekezana baada ya wenzao kuzembea kwenye mazoezi hayo.

Wanacheza mechi ya mazoezi kama vile ni ya mashindano, huku kila upande ukiwa hautaki kupoteza wala kucheza kwa kiwango cha chini.

Ukiachana na ushindani wa kitimu, upo ule wa kumshawishi kocha, hivyo inakuwa ngumu kujua ni kikosi kipi kinaanza katika mechi zilizopita, hilo linasaidia kuondoa uvivu na uzembe.

UMAKINI NA KAZI

Kocha Mwambusi katika mazoezi hayo, alionekana hataki mchezo kabisa linapokuja suala la mchezaji kutimiza majukumu yake kikamilifu.

Alimfuatilia mchezaji mmoja mmoja namna anavyozingatia maelezo anayotoa, alisisitiza umakini alipoona pana udhaifu, alipongeza waliopatia na kuwataka kuongea bidii.

Alisikika akiwaambia baadhi ya wachezaji kwamba wanachokifanya katika mazoezi, wakakionyeshe katika mechi za mashindano.

UTANI KIDOGO

Pia kocha kama mzazi kuna wakati alikausha alipowaona wanataniana, lakini aliwarejesha kwenye mstari akiona utani unawatoa katika umakini wa kazi.

Baadhi ya maneno ya utani ambayo Mwanaspoti lilinasa ya utani, kama mchezaji akitokea amepiga pasi mkaa anaambiwa na wenzake kwamba ajitahidi kula vizuri ili awe na nguvu ya kupiga mashuti.

Wakati mwingine walihamasishana kujituma kwa utani kwani baadhi wakisikika wakiambiana, wapambane wana watoto wanaowategemea.

LAMINE NA KISWAHILI

Enzi za uhai wake, Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli alisisitiza matumizi ya lugha ya Kiswahili kadri iwezekanavyo na hilo ni kama limefanyiwa kazi na beki wa kati wa timu hiyo, Lamine Moro.

Lamine ni ngumu kumgundua kama ni mzungumzaji mzuri sana wa Kiswahili ukikaa naye dakika chache, ila ukitaka kumfaidi kutana naye kwenye anga zake.

Mwanaspoti lilimnasa katika mazoezi hayo, akiwaelekeza wenzake kwa Kiswahili.

Alikuwa mzungumzaji mzuri wa Kiswahili cha ndani, jambo ambalo liliwafurahisha mashabiki ambao walikuwa nje ya uwanja wakishuhudia tizi hilo.

“Oya piga huku....wewe mpe pasi yule..., acheni uzembe nyie....samahani nimekosea bwana...” ni baadhi ya maneno aliyokuwa akitamka Lamine na kama humjui unaweza kusema ni Mbongo kabisa!

MABEKI MZUKA

Katika mazoezi hayo kocha Mwambusi alikuwa anataka kila mtu afunge mabao, ilikuwa hivi, kila beki alikuwa anampigia pasi straika kisha anaanza kumkaba wakati wa kwenda kufunga.

Ilifika zamu ya straika kumpigia pasi beki ili akafunge, hapo ndipo ilitokea kasheshe kupangiwa majukumu kinyume chake, wakaanza kutambiana kila mmoja akijiona bora kuliko mwingine.

Mabeki walianza kuwaambia washambuliaji na mawinga kwamba wakakabe waone ugumu wa kazi zao jinsi zilivyo ngumu na zinavyohitaji umakini mkubwa.

Kati ya mabeki waliosikika wakitamba na wakimwambia mawinga na mastraika kwamba waone ugumu wa kazi hiyo ni Adeyun Saleh na Juma Makapu.

Fiston Abdoulrazack hakutaka kunyamazia tambo zao, alijibu mapigo, huku akimtaja Adeyun kwamba anakwenda kushambulia kama gari bila kuwa na ufundi wa kumkwepa beki.

Kwa upande wa Tuisila Kisinda anayetumia lugha ya Kifaransa, alipokuwa akilalamikia kitu alikuwa akienda kumwambia mkalimani wake, Shikhalo.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz