Uongozi wa Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Young Africans umesema malengo yao ni kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu 2023/24.
Baada ya ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Asas ya Djibout Uwanja wa Azam Complex juzi Jumamosi (Agosti 26), Young Africans itakutana na Al Merreikh ya Sudan ambayo waliitoa Otoho ya Congo-Brazaville na mchezo wa kwanza unatarajiwa kuchezwa Rwanda mwezi ujao.
Afisa Habari wa Young Africans, Ali Kamwe amesema wao kama uongozi malengo yao ni kuingia hatua ya makundi na ili kufika uko ni lazima wapate ushindi dhidi ya Al Merreikh.
“Tunajua uwezo wa wapinzani wetu Al Merreikh pamoja na matatizo yao ya kivita. Lakini ni moja ya timu kubwa Sudan na Afrika na sisi kama Young Africans tumeweka malengo ya kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo hakuna namna zaidi ya kupata ushindi kwenye mechi hiyo,” amesema Kamwe.
Amesema wao kama uongozi jukumu lao ni kusikiliza nini benchi la ufundi la timu hiyo linataka kuweza kufikia lengo hilo na kusisitiza hawaoni sababu ya kushindwa kutimiza adhima yao hiyo kutokana na ubora wa kikosi walichosajili.
Mara ya mwisho Young Africans kufuzu hatua yamakundi ya Ligi ya Mabingwa ilikuwa mwaka 1998 ambapo waliiondoa mashindanoni Coffee ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 8-3 ikiwa ni baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 Addis Ababa na Dar es Salaam Yanga wakaibuka na ushindi wa mabao 6-1.