Kikosi cha Yanga usiku wa jana kilikuwa uwanjani mjini Tunis, Tunisia kumalizana na US Monastir katika mechi ya kwanza ya Kundi D ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini tayari ilishaanza mapema hesabu ya pambano lijalo dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.
Yanga itakuwa wenyeji wa mabingwa hao wa zamani wa michuano hiyo na ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye mechi ya pili ya kundi hilo lenye pia timu ya Real Bamako Jumapili ya wiki hii utakaopigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Mabosi wa Yanga kabla ya kwenda Tunisia kwa mechi ya jana usiku, ilishaweka mipango sawa kwa mchezo huo ujao ikiwamo kuanza kuuza tiketi, sambamba na kuseti kila kitu ili kuhakikisha inaibuka na ushindi nyumbani kabla yakuwafuata Real Bamako mjini Bamako, Mali.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alikakariwa kuwa walianza maandalizi hayo mapema ili kutengeneza mazingira mazuri ya kupata ushindi nyumbani mbele ya Mazembe ambao katika mechi za makundi ya mwaka 2016, iliwatambia nje ndani, kitu ambacho hawakati kitokee tena.
Katika mechi hizo ambazo Yanga ilimaliza mkiani, Mazembe ilianza kwa kushinda jijini Dar kwa bao 1-0 kisha kwenda kutakata Lubumbashi kwa mabao 3-1 na kuwarahisishia kuvuka kwenda robo fainali na mwishowe kwenda kubeba taji hilo kwa kuifumua Mo Bejaia ya Algeria ambao nao walikuwa kundi moja na timu hiyo sambamba na Medeama ya Ghana.
"Mambo ni mengi na muda ni mchache ndio maana mipango imeanza mapema ili tukirudi kutoka Tunisia kumalizie palipobakia kwa mechi hiyo ya nyumbani ambao ni muhimu kwetu kupata ushindi kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutoboa kundini," alisema Kamwe.