Yanga inateswa na mzimu wa miaka 25 tangu ilipocheza mara ya mwisho hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 1998 na mabosi wa klabu hiyo wamekutana jijini Dar es Salaam ili kuweka mambo sawa kwani wanajua wana dakika 180 tu za kukata mzizi wa fitina mbele ya El Merrikh ya Sudan.
Timu hiyo itavaana na Wasudani hao wiki ijayo jijini Kigali, Rwanda kisha kurudiana nao wiki moja baadaye na iwapo itapata matokeo mazuri itatinga makundi, kitu ambacho mabosi wa Yanga wanakitaka na ndio maana katika kikao chao walikubaliana kuongeza posho za bonasi ili mambo yawe mepesi.
Kikao hicho kilichofanyika juzi kilihusisha matajiri watupu wa Yanga wakiwamo vigogo wa klabu hiyo sambamba na Kamati ya Mashindano na kuibua hesabu nyingi kwa msimu huu, ikiwamo mechi hizo mbili za kimataifa kwa kukubaliana kuongeza fedha kwa mastaa wa timu hiyo ili wapigane kufika mbali.
Vigogo hao wa Yanga waliamua kuboresha posho za ushindi kwa wachezaji ili kuwapa mzuka wa kupambana uwanjani kuhakikisha timu inagawa dozi na kuchanja mbuga wakiisaka rekodi zaidi ya ile ya msimu uliopita walipofika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kutetea mataji matatu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo aliliambia Mwanaspoti tayari uongozi wao na kamati yake ipo tayari kuanza msimu wa kupigania heshima ya ushindi kwa klabu yao baada ya mikakati kamili kuwekwa na pande hizo.
Gumbo alisema msimu huu uongozi wao umekusudia kufanya makubwa wakitaka kufidia hatua ya kupoteza taji la Ngao ya Jamii ambako kimataifa na mashindano ya ndani kuna maboresho makubwa ya posho za mechi za ushindi yamefanyika.
Ingawa Gumbo aligoma kuweka wazi viwango vyake akitaka kwanza kutangulia kutangazwa kwa wachezaji, lakini ametamka kwamba kwa viwango ambavyo wameviweka kwa mashindano ya ndani na nje kuna uwezekano mkubwa mastaa wa Yanga wakaishi msimu mzima bila kugusa mishahara kwa matumizi ya kawaida.
“Ni kweli tumekutana, kubwa ni kujipanga na msimu mpya, kuna mengi ambayo tumezungumza, lakini kubwa ni yale ya afya ya timu yetu kufanya makubwa msimu huu ambao tumeuanza kwa kishindo,” alisema Gumbo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga na kuongeza;
“Tumeweka mikakati mingi ambayo hatuwezi kuiweka wazi kwa sababu za kiintelijensia ya klabu, lakini itoshe kusema kwamba kuna maboresho makubwa ya posho tumeyafanya ambayo yatawashangaza wachezaji na kuupigania ushindi kila mchezo.
“Hii Yanga haina mambo ya kuungaunga, nikwambie tu wachezaji wetu msimu huu kazi yao ni moja tu kushinda tena wakimpiga mtu nyingi ndio pesa zinatoka kwa haraka, watakuwa na uwezo wa kuamua kuishi kwa kutegemea hizi posho tu bila kugusa mishahara yao.
“Sitaki kuweka wazi kwa vyombo vya habari kabla ya kuwatangazia wachezaji wenyewe tumetenga kutakuwa na siku maalum ya kwenda kuongea na wachezaji wetu na kikao kitafanyika kabla ya timu kuondoka hapa kwenda Kigali, Rwanda kwa mechi yetu ya kwanza dhidi ya Wasudani.”
Msimu uliopita wachezaji wa Yanga walikuwa wanavuna kiasi kisichopungua Sh100 milioni na kuendelea katika kushinda mechi za kuanzia hatua ya robo fainali ya CAF, huku pia kwa mechi za ndani posho hizo zilikuwa zinaanzia Sh20 milioni hadi Sh300 milioni kutegemea na ugumu wa mchezo wenyewe.
Hivyo kwa kauli hiyo ya Gumbo kupitia kikao hicho cha vigogo ni wazi mastaa wa Yanga watavuna maokoto (fedha) za kutosha iwapo watagawa dozi za maana dhidi ya wapinzani wao iwe wa michuano ya CAF au Ligi Kuu Bara.
Gumbo ambaye ameongoza kamati hiyo kuchukua mataji saba ndani ya misimu mitatu wakifika pia fainali ya Shirikisho Afrika, aliongeza kuwa, kikao hicho kiliridhika na mwanzo mzuri wa kocha wao Miguel Gamondi na hata maboresho ya viwango vya wachezaji.
Yanga imefunga mabao 15 katika mechi tatu zilizopita.