Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga ya Gamondi iko kipindi cha pili

Musonda X Skudu Makudubelaaaa Yanga ya Gamondi iko kipindi cha pili

Mon, 18 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga juzi usiku imeendeleza ubabe kwenye Ligi Kuu Bara kwa kuifumua Mtibwa Sugar kwa mabao 4-1 na kuzidi kuwaweka pabaya mabingwa hao wa zamani wa Tanzania, lakini kilichostua zaidi ni kuimarisha rekodi yao ya kufunga mabao mengi kwenye kipindi cha pili.

Huenda hii ulikuwa hujui, lakini ukweli ni kwamba Yanga ya Kocha Miguel Gamondi imekuwa katili zaidi kwenye kipindi cha pili kulinganisha na kipindi cha kwanza kwenye mechi ilizocheza hadi sasa na kocha huyo amefichua siri ya mabao hayo alipozungumza na Mwanaspoti mara baada ya pambano la juzi.

Mwanaspoti kupitia data ilizonazo, imegundua kuwa, tangu Yanga iwe chini ya Gamondi na kucheza mechi ya kwanza ya kirafiki ya kimataifa ya kuadhimisha Kilele cha Wiki ya Mwananchi kwa kuialika Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, mechi ya ufunguzi rasmi wa msimu huu kwa klabu hiyo, imefunga mabao mengi kipindi cha pili.

Ukihesabu kuanzia mechi hiyo ya Kaizer Chiefs, kisha zile mbili za Ngao ya Jamii, michezo 10 ya Ligi Kuu na saba Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu huu utagundua Yanga imecheza jumla ya mechi 20 na kufunga jumla ya mabao 44, ambapo 14 pekee yamefungwa katika kipindi cha kwanza cha mchezo huku 30 yakifungwa kwenye kipindi cha pili.

Hata katika mchezo wa juzi Yanga iliandika mabao matatu kati ya manne iliyoitungua Mtibwa kwenye kipindi cha pili, huku kile cha kwanza ikifunga moja tu sawa na ilivyoifanyia Simba ilipoifumua mabao 5-1 kwenye Kariakoo Derby.

Katika mchezo huo wa Derby, Yanga ilifunga bao moja kipindi cha kwanza na ilirudi na kasi ya ajabu kipindi cha pili kwa kuitungua Simba mabao manne na kuandika rekodi ya kibabe mbele ya watani hao walioamua kumfuta kazi kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ na wasaidizi wake wawili wakiamini ndio sababu ya kipigo.

MSIKIE GAMONDI

Gamondi aliyeichukua Yanga msimu huu baada ya kocha Nassredine Nabi kuondoka baada ya kuipa Yanga ubingwa wa msimu uliopita, alisema namna ambavyo timu inacheza kwenye mechi ni vile inavyofanya mazoezini hivyo hata mpango wa kupata mabao mengi katika kipindi cha pili ni matokeo ya maandalizi mazuri mazoezini.

“Sio kazi rahisi lakini ni matokeo ya tunachokifanya mazoezini. Timu nyingi ikiwemo sisi, tunatumia kipindi cha kwanza kuangalia mwenendo wa mchezo, ni muda ambao unahitaji kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu bila kuvuruga mfumo na aina yako ya uchezaji wakati huo ukiendelea kumsoma mpinzani.

Kipindi cha pili mara nyingi mambo hubadilika kutokana na kila timu kutaka kujihakikishia ushindi, hapo ndipo unapata utofauti wa mchezo, utabadili wachezaji lakini pia presha itaongezeka na hapo ndipo tunapata mabao. Nawapongeza wachezaji wangu kwa upambanaji wao lakini pia nalipongeza benchi la ufundi kwa kazi kubwa wanayofanya kuhakikisha timu inacheza hivyo bila kuchoka,” alisema Gamondi.

MABAO 30 BARA

Ushindi wa juzi umeifanya Yanga kufikisha pointi 27 na jumla ya mabao 30 katika mechi za Ligi Kuu, ikiwa ni timu ya pili iliyofunga mabao mengi nyuma ya vinara wa sasa, Azam FC yenye pointi 28 na mabao 31.

Katika mabao hayo 30 iliyonayo Yanga, kinara wa orodha ya wafungaji wa ligi na anayeongoza ndani ya timu, Stephane Aziz KI ametupia tisa, akifuatiwa na Maxi Nzengeli mwenye saba, kisha Pacome Zouzoua akifuatia na mabao manne, huku Kennedy Musonda akifunga matatu na Mudathir Yahya (mawili).

Wachezaji wenye bao moja moja ni washambuliaji Clement Mzize na Hafiz Konkoni na mabeki beki Dickson Job na Yao Kouassi, sambamba na winga Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ aliyefunga bao la nne juzi dhidi ya Mtibwa, likiwa ni la kwanza kwake katika ligi tangu ajiunge na timu hiyo kutoka Marumo Gallants ya Sauzi.

MPANGO ULIVYO

Yanga sasa ipo kambini kwake Avic Town, Kigamboni ikijiandaa na mechi ijayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayopigwa keshokutwa Jumatano, ikiwa ni marudiano dhidi ya Medeama ya Ghana baada ya mchezo wa kwanza kutoa sare ya mabao 1-1, ugenini.

Al Ahly inaongoza Kundi D ikiwa na point 5.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: