Mchambuzi wa masuala ya soka nchini kupitia runinga ya TV3, Boiboi Mkali, amesema Yanga inaweza isiwe bora msimu huu kama ilivyokuwa msimu uliopita chini ya Kocha Nasreddine Nabi kutokana na mabadiliko ambayo watayafanya kwenye benchi lao la ufundi.
Boiboi amesema hayo kufuatia Kocha Nabi kuondoka klabuni hapo na klabu hiyo kusajili kocha mpya raia wa Argentina, Miguel Gamondi ambaye alitangazwa juzi kwenye mkutano mkuu wa klabu hiyo.
"Yanga walikuwa bora chini Nabi kwenye misimu miwili iliyopita na kocha huyo ndiye alieijenga timu ya Yanga kuwa katika ubora kwenye kila kitu.
"Kocha mpya akifika kwenye timu ni lazima atake kutambulisha mifumo yake kwa wachezaji na namna anavyohitaji timu icheze, na inawezekana kuna wachezaji wasihitajike na kocha huyo kutokana kutoendana na mifumo ya kocha huyo.
"Inaweza kupelekea timu kushindwa kuwa katika ubora uleule na kupelekea kutopata matokeo mazuri mwanzoni mwa msimu ujao, hivyo mashabiki wa Yanga wajiandae kutokana na mabadiliko hayo," amesema Boiboi.