Wakati Nasreddine Nabi anakuja Yanga SC hakuwa akifahamika sana nchini, hakuanza vyema baada ya vichapo na kuondolewa kwenye mashindano ya kimataifa, Mtunisia huyo aliomba miezi mitatu ya kukisuka upya kikosi hicho, kilichofuata baada ya hapo ni historia.
Hofu ya mashabiki wengi ni kama Kocha Miguel Gamondi ataweza kuifikisha Yanga pale alipoiacha hususani michuano ya kimataifa, lakini wasisahau kuhusu ukubwa wa Gamondi na mwanzo wa Nabi.
Kwani Gamondi baada ya mchezo wa Jumamosi dhidi ya Kaizer Chiefs ameleta taswira mpya kwa klabu hiyo. Falsafa ya Gamondi na muundo wake ni kama ameishi kwenye falsafa ya Wananchi.
Wacha nikusanue kitu kuhusu uchezaji wake na walichokifanya wachezaji kwenye mchezo wa Jumamosi.
Kuanzia kwa kipa Metacha Mnata amekuwa mtulivu sana golini, soka la Gamondi linafanya timu ikae na mpira muda mwingi, ameongeza kasi kwenye muundo wake na faida yake kubwa ni wachezaji kama Khalid Aucho, Mudathir Yahaya na wengine ambao wameiishi mifuno ya Nabi.
Utulivu wa mabeki wakiongozwa na nahodha wao Bakari Mwamnyeto, wanapandisha mashambulizi kwa weredi na kwa kufuata mfumo ambao mwalimu anautaka. Wanakaba kwa nidhamu na kila mtu unamuona anatimiza majukumu yake kwa asilimia kubwa.
Skudu Makudubela na Max Nzengeli wameingia moja kwa moja katika muundo wa mwalimu, kama atahitaji kasi na unyumbulifu basi amepata watu sahihi, wamecheza mechi kwa ufanisi mkubwa kama waliishi na kocha Morocco.
Chrispin Ngushi wa Gamondi amekua Fiston Mayele wa Nabi kwenye mchezo wa Jumamosi, amekua na ustadi, nguvu na kasi sana hii itamfanya apambane na Kennedy Musonda ambaye ndiyo mshambuliaji kiongozi kwa sasa.
Yanga watammisi Mayele ya mitetemo yake, Mayele na uwezo wake wa kucheka na nyavu lakini maeneo yote yapo salama na Gamondi kaanza kuonyesha sura mpya. Muendelezo wake utamfanya kuimbwa kama Mond na midundo yake.