MASHABIKI wa Yanga wana kila sababu ya kutembea vifua mbele na kufagilia chama lao. Sio kwa sababu ya kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara, lakini ukweli ni kutokana na kuonekana kuwa moto kuliko msimu uliopita.
Yanga ya msimu huu imeonekana kuwa moto zaidi kwani katika mechi zao 12 za Ligi Kuu Bara wameifunika kabisa rekodi yao ya msimu uliopita kwa idadi ya mechi kama hizo.
Katika mechi hizo 12 za msimu huu, Yanga imeshinda mechi 10 na kutoka sare mbili, ikifunga mabao 22 ya kufunga na kufungwa manne, huku ikikusanya pointi 32, wakati msimu uliopita wababe hao walivuna pointi 28 tu.
Sio pointi 28, lakini pia ilifunga mabao 14 na kufungwa mabao manne ikishinda mechi nane na kupata sare nne, japo ilikuwa haijapoteza kama msimu huu na pia ilikuwa kileleni kama sasa ikiitangulia Simba.
Licha ya Yanga iliongoza msimamo hadi raundi hiyo ya 12 na kuendelea kutesa kileleni, lakini mwisho wa msimu ulimaliza ligi ikiwa na pointi 74 katika nafasi ya pili, huku watani wao, Simba ikibeba ndoo kwa pointi 83 kila moja ikicheza mechi 34.
Katika mechi kama hizo kwa msimu uliopita, Simba ilikuwa na pointi 23 na mabao 26, lakini kwa sasa imeonekana kuwa imara zaidi licha ya juzi kati kufumuliwa 1-0 na Mbeya City, kwani imekusanya pointi 24 katika mechi 11 tu.
Hata hivyo kasi ya ufungaji kwa Simba imepungua kwani msimu huu imefunga mabao 14 na kuruhusu matano, ikizidiwa na Yanga mabao nane na pointi nane.
YANGA RAUNDI 12 (2020/21)
Yanga 1-1 Prisons (pointi 1), Yanga 1-0 Mbeya City (pointi 3), Kagera Sugar 0-1 Yanga (pointi 3), Mtibwa Sugar 0-1 Yanga (pointi 3), Yanga 3-0 Coastal Union (pointi 3), Yanga 1-0 Polisi Tanzania (pointi 3), Yanga 1-1 Simba (pointi 1), KMC 1-2 Yanga (pointi 3), Biashara United 0-1 Yanga (pointi 3), Gwambina 0-0 Yanga(0), Azam FC 0-1 Yanga (pointi 3) na Yanga 1-1 Namungo (pointi 1).
SIMBA POINTI 23 (2020/21)
Ihefu 1-2 Simba (pointi 3),Mtibwa Sugar 1-1 Simba (pointi 1),Simba 4-0 Biashara United (pointi 3), Simba 3-0 Gwambina (pointi 3),JKT Tanzania 0-4 Simba (pointi 3),Tanzania Prisons 1-0 Simba (0), Young Africans 1-1 Simba (pointi 1), Simba 0-1 Ruvu Shooting (0),Simba 2-0 Kagera Sugar(pointi 3),Dodoma 1-2 Simba (pointi 3) na Coastal Union 0-7 Simba (pointi 3).
WABOBEZI WAZUNGUMZIA
Akizungumzia suala hilo, kipa wa zamani wa Simba, Steven Nemes alisema Yanga kufunga mabao 22 katika raundi 12, imezidisha idadi ya mabao nane katika 14 waliyofunga msimu ulioisha.
“Inaonyesha wana kikosi kizuri cha washambuliaji, lakini kuhusu kuongoza ligi, msimu ulioisha waliongoza kwa muda mrefu, wakaja wakapinduliwa na Simba, hivyo ni jambo la kungojea nani atakuwa bingwa,” alisema.
Kiungo wa zamani wa Yanga, Salvatory Edward alisema timu hiyo kuvunja rekodi yake ya msimu ulioisha katika raundi ya 12, inaonyesha namna ambavyo njia ya ubingwa ni wazi kwao.
“Yanga ya msimu huu siyo ya mchezo kabisa, ingawa bado ligi ni ngumu, lakini wachezaji wanapaswa kukomaa na kutoacha mpenyo kwa timu iliyo nafasi ya pili,” alisema.