JANA jioni wakati nyota wa Yanga na makocha wao wakiongozwa na Nasreddine Nabi wakiendelea kupiga tizi la mwisho kabla ya kuvaana na Simba, kambi yao ilipata ugeni uliokuja na neema iliyowajaza mzuka mastaa hao kwa mchezo huo wa Kariakoo Derby.
Vigogo wa Yanga wakiongozwa na wadhamini wao kutoka GSM pamoja na wajumbe wa kamati ya mashindano, waliibukia wachezaji wao ili kuwapa morali zaidi kwa mchezo wa leo utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, kuanza saa 11:00 jioni kisha kuwaambia; “Tunataka ushindi tu kesho (leo).”
Wakati wachezaji wakipanga cha kujibu, wakashtukizwa na sapraizi ya ahadi nono ya bonasi, iliyowafanya wengi wao kushindwa kuzuia na kulipuka kwa furaha kabla ya kujibu kwa kujiamini. “Msiwe na hofu, hao tutawamaliza mapemaa.”
Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa, vigogo hao waliamua kutimba kambini saa 10 jioni kuangalia tizi la mwisho, lakini pia kuendelea kuwatia hasira nyota wao ili kuizima Simba leo katika mechi ambayo kama watateleza watajitia aibu ya kugeuzwa ngazi ya kuwapata watani wao ubingwa.
Inaelezwa, kambi ya Yanga mzuka umepanda wakiamini kabisa leo wanaenda kumaliza kazi mapema, licha ya ukweli wapinzani wao wanaonekana kujiamini kutokana na kuongoza msimamo kwa tofauti ya alama sita, huku wakiwa na mechi za viporo mkononi.
Wachezaji wa Yanga waliahidi mbele ya vigogo hao kwamba leo Mnyama hachomoki Kwa Mkapa kwa vile hawataki kutumika kuwapa taji la nne mfululizo watani wao ambao kama wakishinda watatangaza ubingwa kabla msimu haujamalizika, wakiwa na michezo minne mkononi.
“Wachezaji wana morali kubwa na wanaamini Simba hawatoki salama, kwa namna walivyoandaliwa na Kocha Nabi,” kilisema chanzo chetu.
Rekodi zinaonyesha kwa mechi tatu zilizopita za Ligi Kuu Bara, Simba haijapata ushindi wowote zaidi ya kipigo kimoja na sare mbili, huku rekodi za jumla zikiibeba Jangwani katika mechi zao 105 tangu 1965 katika Ligi ya Bara, kwani imeshinda mechi 37 dhidi ya 31 walizoshinda Simba huku sare zikiwa 37.