Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga wavunja rekodi zao wenyewe

Yanga Paradesz Yanga wavunja rekodi zao wenyewe

Thu, 30 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

HUKU ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa misimu mitatu mfululizo, Yanga imefanikiwa kuvunja rekodi zake za msimu uliopita, huku watani zao wa jadi Simba wakishindwa kufanya hivyo, ikiishia nafasi ya tatu kwenye msimamo.

Kwa mujibu wa dawati letu la takwimu, Yanga ambayo imekata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, imemaliza mechi zake 30 msimu huu ikijikusanyia pointi 80, na kuvunja rekodi ya msimu uliopita ilipomaliza ikiwa na pointi 78, hivyo msimu huu imezidi pointi mbili zaidi.

Msimu huu, Yanga imemaliza ligi ikishinda michezo 26, hivyo kuvunja rekodi ya msimu uliopita iliposhinda michezo 25, ambapo imezidi mchezo mmoja mbele.

Mabingwa hao msimu huu wameongeza idadi ya mabao 10 zaidi ya msimu uliopita, kwani wamepachika mabao 71, wakivunja rekodi ya msimu uliopita, walipomaliza na mabao yao 61, huku pia ikiruhusu idadi ndogo ya mabao ambayo ni 14 tu, wakati msimu uliopita iliruhusu mabao 18, hivyo kuwa pungufu ya mabao manne msimu huu.

Rekodi nyingine ya kujivunia kwa Yanga msimu huu ni kushinda mechi zake zote 15 nyumbani, huku ikipata sare mechi tatu ugenini na kupoteza mechi mbili.

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, akizungumza muda mfupi baada ya kumalizika kwa ligi hiyo juzi, alisema wamekuwa na msimu bora, wakiweka na kuvunja rekodi nyingi, akiisifu timu yake kuwa ilikuwa timu ya kutisha msimu huu.

"Tumetengeneza rekodi nyingi na tumevunja rekodi nyingi msimu huu, tumepata pointi nyingi sana, tumefunga mabao ya kutosha na tumeruhusu mabao machache, sitaki kuzungumzia 'hat-trick' hapa wala 'asisti', rekodi hizo za klabu zinatosha kuonyesha tulikuwa timu bora," alisema Gamondi.

Kwa upande wa Simba ambayo msimu huu imeshika nafasi ya tatu, ikiambulia kucheza Kombe la Shirikisho msimu ujao, imeshindwa angalau kufikia rekodi yake iliyoweka kwenye Ligi Kuu msimu uliopita, achilia mbali kuvunja.

Imemaliza Ligi ikiwa na pointi 69, pointi nne nyuma ya zile ilizopata msimu uliopita ambapo ilivuna pointi 73, huku pia msimu huu ikiruhusu mabao 25, manane zaidi ya msimu uliopita, iliporuhusu mabao 17 tu.

Timu hiyo msimu huu imepata ushindi mara 21, ikishindwa kuifikia rekodi ya msimu uliopita iliposhinda mara 22, pia msimu uliopita ilipoteza mchezo mmoja tu, msimu huu imepoteza mechi tatu.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alikiri kuwa haukuwa msimu mzuri kwa sababu hawakutimiza malengo yao.

"Msimu huu hatukutimiza malengo yetu kwa asilimia 90, lakini huo ndiyo ushindani, tuna nafasi kubwa ya sisi wenyewe kujiangalia wapi tumekosea, ukiangalia sehemu kubwa ya makosa tuliyoyafanya ni yetu sisi wenyewe, inabidi sasa kukaa na kuangalia wapi pa kurekebisha ili msimu ujao turejee tukiwa bora zaidi," alisema Ahmed.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: