Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga wautaka ubingwa

20e721db2677566deda0fe00e9f87005 Yanga wautaka ubingwa

Mon, 24 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KLABU ya Yanga imeendelea kufunika katika jiji la Dodoma wakati ikizundua wiki wa Mwananchi, huku wakitaka ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara waliokosa kwa misimu mitatu mfululizo.

Baada ya kufanya shughuli mbalimbali, ikiwemo kuzindua matawi, kufanya usafi na kuzunguka katika mitaa mbalimbali ya Dodoma, mwenyekiti wa Yanga , Dk Mshindo Msolla sasa wanautaka ubingwa.

Dk Msoll alisema timu yao msimu huu itakuwa moto baada ya kusajili vizuri tofauti na mwaka jana, ambapo usajili wao ulikuwa wa kuungaunga kutokana na kutokuwa na fedha.

Alikiri kuwa Yanga haikufanya vizuri mwaka jana na hiyo ilitokana na kushindwa kufanya usajili wa maana katika dirisha kubwa na ikawa vigumu kurekebisha makosa hayo katika dirisha dogo.

Msolla alisema kuwa unaposhindwa kusajili vizuri katika dirisha kubwa, basi usitarajie kurekebisha ma kosa hayo kupitia kipindi cha usajili cha dirisha dogo, kwani inakuwa ngumu kurekebisha.

Alisema msimu uliopita Yanga haikusajili vizuri dirisha kubwa, lakini pamoja na kusajili wachezaji wengi katika dirisha dogo, wameshindwa kupata mafanikio.

Alisema mwaka jana GSM ilisaidia kusajili wachezaji watano na mwanachama mmoja alisajili mmoja.

Aliipongeza Kampuni ya GSM kwa kuendelea kugharamia kambi ya timu hiyo kwa asilimia 100 tangu mwaka jana na inaendelea kufanya hivyo hadi sasa.

Alisema Yanga hawajawahi kugombea mchezaji na Simba zaidi ya Bakari Mwamnyeto na vijana hao wa Jangwani waliibuka washindi kwa kumsajili mchezaji huyo na wala sio mwingine.

Alisema wachezaji saba wa nyumbani na watano wa kigeni wote wamesajiliwa na GSM hadi sasa, ambapo aliwataka wanachama kutoa ushirikiano kwa benchi la ufundi ili lifanye vizuri.

Aliwataka wanachama wa Yanga kuchangia ili kuhakikisha wana wasajili wachezaji wawili wa nje, ambapo alisisitiza kuwa wachezaji hao wako tayari na kinachosubiriwa ni fedha tu.

Alisema msimu ujao wanataka kufanya vizuri na lengo lao ni kutwaa ubingwa, huku akiwataka wanachama kujitoa zaidi kuichangia timu hiyo ili iweze kufanikisha lengo hilo.

Alisema kila safari ya timu kwenda mkoani, kuanzia sasa kutakuwa na mchezaji wazamani ili kuwahamasisha wachezaji kuhusu umuhimu na ukubwa wa Yanga.

Aidha, Msolla alitumia wakati huo kutangaza kuwa Yanga imepata kocha mpya, Cedric Kaze ambaye atawasili nchini wakati wowote akitokea Canada, ambako alikuwa akifanyakazi.

Shamrashamra za wiki ya Mwananchi zitafikia kilele Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya kuzinduliwa Dodoma, na Yanga itacheza na timu kutoka nje ya nchi.

Chanzo: habarileo.co.tz