Yanga juzi imetua nchini Mali tayari kwa dakika 90 dhidi ya wenyeji wao, Real Bamako ya huko lakini makocha wana nondo nne, ili kuhakikisha wanashinda ugenini kwa mara ya kwanza kundini.
Kwanza wataicheza mechi hiyo kama fainali, pili watadhibiti kasi ya wenyeji, tatu watakuwa makini na kucheza faulo zitakazowapa nafasi Real Bamako ambao ni mafundi wa mipira hiyo, lakini mwisho watahakikisha wanashinda mechi hiyo kwani ni ya kufa au kupona lakini kuwatumia nyota wao kumaliza kazi kama ilivyofanywa kwa TP Mazembe waliyoifunga mabao 3-1.
Lakini vilevile, wamewasisitiza wachezaji wao kuwa makini na viungo na mawinga wa wenyeji. Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwanaspoti kabla ya kuondoka nchini makocha wa timu hiyo, Nasreddine Nabi na msaidizi wake, Cedric Kaze, walisema wanakwenda kucheza mechi hiyo kama fainali dhidi ya Bamako kwani timu zote mbili zinahitaji kujua njia yao ya kufuzu au kutofuzu.
“Hii ni fainali kwetu lakini hata wao pia, sisi tumeshinda mechi moja na tukapoteza moja na wao wamepoteza moja na kutoa sare moja, watahitaji ushindi ili kufufua hatma yao na sisi tunahitaji ushindi ili tujiweke salama zaidi, hii ni mechi ambayo itaamua safari yao na yetu,” alisema Nabi.
“Tunawajua Bamako, wana viungo wazuri, pia mabeki wao wa pembeni ni hatari kama tukifanya makosa ya kuwafanya wawe huru, tutakuwa na mechi ngumu lakini tunataka kusahihisha makosa yetu ya kupoteza ugenini,” aliongeza kocha huyo kutoka Tunisia.
Kaze alisema kasi ya Real Bamako lazima idhibitiwe ili kurahisisha kuusaka ushindi kwa kutumia morali ya kikosi kilichowachapa TP Mazembe ili kuwapa nguvu wachezaji kujiamini na kuongeza umakini.
“Tunawajua Bamako wana kasi pia katika kutengeneza mashambulizi yao na pia kutumia mipira iliyokufa, hili tunalijua tunatakiwa kujipanga kulidhibiti vyema,” alisema Kaze ambaye hivi karibuni aliitosa ajira ya kuifundisha timu ya taifa analotoka la Burundi.
“Tunataka kutumia mechi hii kujiimarisha zaidi katika malengo yetu ya kundi letu kufika mbali tunajua kwamba nao watahitaji ushindi kitu kikubwa ni kuwa makini zaidi. Lakini tunaenda tukiwa na mbinu za kuhakikisha tunashinda ugenini kwa mara ya kwanza kundini.”
Yanga itakuwa wageni wa Real Bamako Jumapili ya wikiendi hii mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Machi 26 (Stade du 26 Mars), baada ya awali kufungwa 2-0 ugenini na US Monastir ya Tunisia.