Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga wapewe maua yao

Yangas Aziz Kiii Yanga wapewe maua yao

Tue, 18 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwezi uliopita tulishuhudia historia nchini katika anga la michezo hususani mchezo wa mpira wa miguu ikiandikwa baada ya Yanga kutangaza ubingwa wao wa 30 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ni ubungwa wa tatu mfululizo ndani ya miaka mitatu wakipokea kijiti cha ubingwa kutoka kwa Simba waliotawala kwa misimu minne mfululizo.

Yanga imekuwa na mafanikio makubwa kwenye misimu hiyo huku ikafanya vizuri pia kwenye mashindano ya kimataifa, ikitinga fainali ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita na hatua ya robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika msimu huu.

Mafanikio hayo ya Yanga hayakufikiwa kimiujiza; imefika hapo kutokana na uwekezaji mzuri na bora, ikiongozwa na viongozi wenye maono mapana kwenye soka.

Hakuna ubishi uongozi wao chini ya Rais Hersi Said umesaidia kufika walipofika sasa na kushinikiza mafanikio waliyonayo sasa.

Pamoja na upinzani na ubishani wa kimichezo, Yanga wanastahili pongezi na kuwa mfano kwa klabu nyingine katika kufikia mafanikio waliyonayo sasa. Zipo klabu nyingi ambazo zinapaswa kuiga mfano wa Yanga kwenye kujiendesha, usajili na hata maandalizi yao kuelekea msimu husika wa mashindano. Mafanikio waliyonayo Yanga katika kipindi cha miaka mitatu yanatokana na uongozi bora pamoja na mwekezaji mwenye kiu ya mafanikio.

Rais wao ni kiongozi kijana mwenye maono, tamaa na kiu ya mafanikio na ndio maana hata akapigiwa kura kuwa Mwenyekiti wa Vilabu vya Soka Afrika.

Kwa viongozi wengine, si vibaya kuiga na kuwa na kiu ya mafanikio haya waliyofikia Yanga chini ya Hersi na sekretarieti yake. Kwa uongozi wake na uimara wa klabu hiyo, haitashangaza kusikia msimu ujao wametwaa tena ubingwa wa Ligi Kuu na kufika mbali kwenye michuano ya Afrika.

Tusidanganye, uongozi imara na uchumi madhubuti wa klabu ndio kichocheo kikubwa cha mafanikio kwenye soka.

Timu nyingine zinapaswa kuiga mafanikio haya ya Yanga ambayo hata hivyo hayajaja mara moja, ni mchakato ulioanza miaka minne nyuma kabla ya kuchukua ubingwa kutoka kwa Simba.

Wakati Simba wakiwa kwenye kilele cha mafanikio, Yanga walikuwa wanakuna kichwa kuona ni namna gani wanaweza wakafikia mafanikio ya watani.

Baada ya mchakato huo wa muda mrefu, Yanga wamekuwa vizuri kwenye michuano ya ndani na nje. Kwa mara ya kwanza msimu uliopita tumeshuhudia  timu hiyo ikicheza hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya milongo mingi.

Msimu mmoja nyuma, Yanga hiyo hiyo ilishuhudiwa ikicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Haya ni mafanikio makubwa.

Tusibeze mafanikio haya, kuna kila sababu ya kuwapongeza Yanga hususani viongozi wao kwa kile wanachokifanya. Klabu nyingine ziige njia za viongozi wa Yanga kwenye kuiletea timu mafanikio.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live