Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga wapewa ramani ya ushindi, uamuzi unabaki kwao

Yanga2g Kikosi cha Yanga

Fri, 17 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Timu ya Yanga wakijiandaa kuwavaa wababe kutoka Congo TP Mazembe mchezo wa hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Afrika jumapili hii katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Bado Mastaa wa zamani waliocheza Soka nchini wameendelea kutoa ushauri kwa Yanga jinsi ya kushinda mchezo huo.

Straika wa zamani wa Yanga, Boniface Ambani ameipigia chapuo timu hiyo kuibuka na ushindi katika mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe.

Kikosi cha Yanga kilichopo Kundi ‘D’ kilitua nchini jana kikitokea Tunisia ambako kilifungwa mabao 2-0 na US Monastir huku wapinzani wao - TP Mazembe wakishinda mchezo wa kwanza kwa mabao 3-1 dhidi ya Real Bamako ya Mali.

Akizungumza kutoka jijini Nairobi - Kenya, Ambani ambaye aliwahi kuonyesha uwezo mkubwa akiwa Yanga alisema jambo kubwa ambalo wachezaji wa timu hiyo wanapaswa kulifanyia kazi ni kushambulia kuanzia mwanzo wa mchezo akiamini njia hiyo itakuwa ni silaha ya ushindi.

“Wasahau matokeo yaliyopita na akili zao waziwekeze kwa Mazembe kwa sababu timu nyingi zilizopata ushindi zilitumia vizuri uwanja wao wa nyumbani,” alisema.

“Hivyo hilo ni jukumu wanalopaswa kulizingatia. Siwashauri wakae nyuma kwa kuwa wakipata sare haiwezi kuwasaidia kama kupata ushindi.

“Mbali na kushambulia ila nidhamu pia inahitajika kwenye uzuiaji kwa sababu Mazembe ni wazoefu na timu za Tanzania na isitoshe zimewahi kukutana kwenye michezo hii ya CAF na Yanga ikapoteza michezo yote miwili.”

Yanga na Mazembe zinakutana zikiwa na kumbukumbu ya kipekee kwani ziliwahi kukutana kwenye michuano hii mwaka 2016, zikiwa kundi ‘A’ sambamba na timu za Medeama ya Ghana na Mo Bejaia ya Algeria.

Juni 28, 2016 Yanga ikiwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ilikubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa TP Mazembe lililofungwa na Merveille Bokadi katika dakika ya 74 kwenye mchezo wa awali wa hatua ya makundi.

Katika mchezo wa marudiano uliopigwa Agosti 23, 2016, Yanga ilifungwa mabao 3-1 yaliyofungwa na Jonathan Bolingi na Rainford Kalaba aliyetupia nyavuni mara mbili huku lile la Yanga la kufutia machozi likifungwa na Amissi Tambwe.

Kwenye kundi hilo, Yanga ilimaliza katika nafasi ya nne na pointi nne nyuma ya vinara - TP Mazembe waliomaliza na alama 13 huku Mo Bejaia ikimaliza ya pili na pointi nane sawa na Medeama iliyomaliza ya tatu timu hizo zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live