Mchambuzi maarufu wa masuala ya soka nchini kupitia kituo cha runinga cha TV3, Alex Ngereza amedai kuwa Klabu ya Yanga wanaweza kumpoteza kwenye mchezo, winga wao Maxi Mpia Nzengeli raia wa Congo DR baada ya kujipata matarajio makubwa juu yake.
Ngereza amesema hayo mara baada ya Yanga kutangaza kuwa kwenye mchezo wa leo wa Kinataifa dhidi ya ASAS FC ya Djibouti wameupa jina mchezo huo kama 'Maxi Nzengeli Day' ikiwa ni sehemu ya kuweka hamasa kwa wachezaji wao.
"Sikuona sababu ya Yanga kuita "MAX DAY" mechi yao ya marudiano na Asas hii itampa presha kubwa sana mchezaji na inaweza kumtoa mchezoni Max,Yanga wasisahau tofauti ni goli mbili tu na kwenye mchezo wa mpira chochote kinawezekana," amesema Ngereza.
Mchezo wa leo utapigwa saa 1:00 katika Dimba la Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam huku Yanga wakipewa nafasi kubwa ya kusonga mbele.
Katika mchezo wa kwanza Yanga walifanikiwa kushinda bao 2-0 hivyo kwa leo wanahitaji kupata sare yoyote ili waweze kusonga mbele katika hatua inayofuata ya michuano ya CAFCL.