Yanga imekuwa na kismati inapochezeshwa mechi za Ligi Kuu na mwamuzi Omary Mdoe kutoka Tanga ambaye juzi usiku alikuwa kati wakati vijana wa Miguel Gamondi wakiinyoosha KMC kwa mabao 5-0.
Rekodi zinaonyesha kuwa chini ya mwamuzi huyo vigogo hivyo havijawahi kupoteza mchezo wowote.
Mchezo wa juzi ambao Yanga ilishinda kwenye Uwanja wa Azam Complex dhidi ya KMC ulikuwa ni wa kwanza kwa mwamuzi huyo kwa msimu huu, lakini ukiwa ni wa nne kuichezesha timu hiyo kwani msimu uliopita alichezesha michezo mitatu.
Kwa msimu uliopita, Mdoe alianza kuichezesha Yanga dhidi ya Ihefu na ikashinda bao 1-0 mechi iliyopigwa Januari 16, kisha Aprili 11 alikuwa kati wakati Yanga ikiifumua Kagera Sugar kwa mabao 5-0 na Mei 13 wakati Yanga ikitangaza ubingwa iliifumua Dodoma Jiji mabao 4-1.
Katika michezo minne Mdoe aliyoichezesha Yanga imeshinda yote huku ikifunga jumla ya mabao 15 na kuruhusu matatu tu.