Mchambuzi nguli wa masuala ya soka nchini, Edo Kumwembe amesema kuwa Klabu ya Yanga kupitia benchi lao la ufundi linaloongozwa na Kocha Miguel Gamondi watakuwa wamepata somo kubwa na mbinu za namna ya kucheza na mabingwa wa muda wote wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly.
Edo amesema hayo kuelekea mchezo wa hatua ya makundi ya michuano hiyo kati ya Yanga na Ahly utakaopigwa Jumamosi ijayo, Desemba 2, 2023 katika Dimba la Benjamin Mkapa jijini dar es Salaam ikiwa ni takribani mwezi mmoja tangu Ahly walipotua nchini kuja kucheza na Simba SC katika mchezo wa ufunguzi wa michuano ya African Football League.
“Yanga wanatazamiwa kuwakaribisha Al Ahly pale Temeke katika mwanzo mpya wa Desemba.
“Matazamio makubwa kwa Wanayanga ni kwamba wanaweza kushinda pambano hilo hasa baada ya kutazama mechi mbili za mwisho za watani wao Simba dhidi ya Al Ahly ambazo zote mbili ziliisha kwa sare katika michuano mipya ya African Football League (Super League).
“Chochote ambacho kinaweza kutoka kando ya pambano hilo kisiwe kufungwa kinaweza kuwasadia Yanga lakini wakifungwa basi watakuwa na mlima mkubwa wa kupanda kuweza kutinga robo fainali yao ya kwanza ya michuano hii tangu mwaka 1998. Zamani sana.
“Nje ya hapo watakuwa wametanguliza mguu mmoja nje kuelekea katika mlango wa kutokea katika michuano hii,” amesema Edo Kumwembe.