Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga wamefungua mlango ambao hawawezi kuufunga tena

Hersi Na Aziz Ki Yanga wamefungua mlango ambao hawawezi kuufunga tena

Wed, 19 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Taarifa za kikachero zinasema Yanga SC wamembakisha staa wao Stephane Aziz KI, ni suala la muda tu kuonesha picha zake akisaini mkataba mpya. Ni taarifa nzuri kwa wanazi wa Yanga. Ni taarifa nzuri kwa mastaa wengine wa Yanga.

Nitakufafanulia hii neno taarifa nzuri kwa mastaa wengine wa Yanga. Njia ya kupambana na kina Al Ahly, Mamelodi na wakubwa wengine wa Afrika ni kufanya hiki walichokifanya Yanga kwa Aziz.

Yanga wamezitanua mbavu zao kisawasawa kumbakisha Aziz. Mchezaji aliyefanya vyema, tena katika level kubwa kama ile ya Aziz mara nyingi ni ngumu kubakia nchini. Lakini Yanga wamembakisha na maisha mengine yanaendelea kama kawaida.

Aziz kubakia kuna mahala Yanga wametuma ujumbe. Bila shaka ujumbe umefika. Timu za juu yetu zilizoea kuja huku kwetu chini kufanya fujo za usajili kadri zilivyotaka. Mara hii wamekutana na ugumu.

Haikuwa kazi rahisi Aziz kubakia. Tayari mkononi mwake alikuwa na ofa nyingine nono. Ndani ya Yanga vilifanyika vikao vya kila mara. Vikao vya simu. Vikao barua pepe (email). Ni vikao vilivyojaa ushawishi.

Mwisho wa siku kijana kachukua kalamu kusaini miaka miwili. Wakubwa huwa hawatamani kuona mchezaji kama Aziz anaendelea kubakia Yanga. Kwao sio afya, huwa wanatamani kila siku timu zetu zianze upya.

Unapombakisha Aziz ina maanisha unaanza kuwasogelea. Hiki ndicho hawakitaki, hawakipendi. Turudi pale kwenye taarifa nzuri kwa mastaa wa Yanga. Kivyovyote vile huko walikokuwa kina Nzengeli Max wamefurahia Aziz kubakia.

Wanajua ukifanya vyema kiwanjani, ukienda mezani kutamka pesa unayotaka unapewa. Huu ndiyo mlango walioufungua Yanga. Ni mlango ambao ni ngumu kuufunga tena. Kila mchezaji atakuja mezani kutaka mkataba mpya kwa ‘Reference’ ya Aziz nae akitaka dau nono na mshahara mkubwa. Kila mmoja atashikia hapo.

Mchezaji akiambiwa timu haina fedha ataona uongo. Ataona mchango wake umepuuzwa ndiyo maana yeye kaambiwa timu haina fedha, lakini Aziz kapewa fedha. Kuna kamtihani fulani hivi Yanga lazima wajiandae nao katika kila dirisha la usajili linapokuwa wazi kuanzia sasa. Yanga wameyavulia maji nguo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live