Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga wamecheza boli, Waarabu wameweka kambani

CR Belozdad V Yanga Yanga wamecheza boli, Waarabu wameweka kambani

Sat, 25 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Licha ya Yanga kupoteza kwenye mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mabao 3-0 dhidi ya CR Belouizdad, Miguel Gamondi na vijana wake wameonyesha wana kitu baada ya kutawala sehemu kubwa ya mchezo huo huku makosa yao ya kupoteza mipira, mbinu sahihi za wenyeji za kushambulia kwa kushtukiza na maamuzi ya utata vikiwanyima Wananchi nafasi ya kuambulia hata bao la kufutia machozi kwenye Uwanja wa July 5, 1962.

Yanga ilimaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza ikiwa na asilimia 61 za umiliki wa mpira dhidi ya 39 za wenyeji, lakini haikuwaokoa kutanguliwa 2-0 hadio wakati wa mapumziko.

Wakaruhusu bao jingine la shambulizi la kushtukiza katika dakika za majeruhi na kujiweka katika wakati mgumu katika mechi yao ijayo nyumbani dhidi ya mabingwa mara 11 wa Afrika, Al Ahly kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Desemba 2.

Kipindi cha kwanza Pacome Zouzoua aliangushwa ndani ya boksi lakini wakanyimwa penalti, baadaye beki Yao Yao aliamuliwa kuwa ameotea kimakosa kama ilivyotokea kwa Kenedy Musonda ambaye aliutumbukiza mpira wavuni lakini mwamuzi msaidizi akaamua kwamba ameotea. Tukio la Yao kudaiwa ameotea lilimkera hata kocha Miguel Gamondi ambaye alimlazimisha mwamuzi kusimamisha mchezo na kwenda kumpa ufafanuzi wa jambo hilo.  

Pamoja na kutawala mchezo, wachezaji wa Yanga walikuwa wakipoteza sana mipira na jambo hilo lilichangia katika kipigo hicho kizito katika mechi yao ya kwanza ya makundi la Ligi ya Mabingwa Afrika ndani ya miaka 25.

Kipa wa Belouizdad, Alexis Guendouz alipangua mashuti ya Mudathir Yahaya na Maxi Nzengeli mapema kipindi cha kwanza, lakini alikuwa ni kipa Metacha Mnata ambaye aliruhusu mabao katika mashuti yote mawili ya wenyeji yaliyolenga lango kipindi cha kwanza.

Katika mechi nyingine ya Ligi ya Mabingwa iliyochezwa mapema jana, wenyeji Pyramids ya Fiston Mayele ilishinda bao 1-0 dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo katika mechi ya kundi A, bao la Fagriye Lakay aliyetumia vyema asisti ya straika huyo wa zamani wa Yanga. 

Chanzo: www.tanzaniaweb.live