Klabu ya Yanga imetumia dakika 170 kuziona nyavu za Kagera Sugar kwa bao la Mudathir Yahya dakika ya 82 akipokea pasi kutoka kwa Stephane Aziz Ki. Mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliomalizika kwa Yanga kuichapa Kagera bao 1-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Bao hilo la Mudathir limekuwa la tisa kwake katika ligi msimu huu akiwa na kikosi hicho akiwafikia nyota wenzake, Maxi Nzengeli aliyefunga idadi ya mabao kama hiyo.
Mchezo wa mzunguko wa kwanza baina ya timu hizo uliopigwa Uwanja wa Kaitaba Bukoba uliisha kwa suluhu Februari 2, mwaka huu.
Hata hivyo mechi ya mwisho baina ya timu hizi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Yanga ilishinda mabao 5-0, Aprili 11, mwaka jana yaliyofungwa na Stephane Aziz KI aliyefunga matatu 'Hat-trick', huku nyota wa zamani wa kikosi hicho, Fiston Mayele na Bernard Morrison wakifunga moja kila mmoja wao.
Mchezo wa mwisho kwa Kagera Sugar kuifunga Yanga katika Ligi Kuu Bara ulikuwa ni ushindi wa mabao 3-0, ikiwa chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Luc Eymael mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam Januari 15, 2020.
Tangu Januari 15, 2020, Kagera imecheza michezo tisa mfululizo ya ligi bila ya kuonja ladha ya ushindi dhidi ya Yanga ambapo kati ya hiyo imepoteza saba na kutoka sare miwili.
Mchezo uliozalisha mabao mengi baina ya timu hizo ulikuwa ushindi wa Yanga wa mabao 6-2, Oktoba 22, 2016 kwenye Uwanja wa Kaitaba huku ikishuhudiwa viongozi wa Kagera wakiwasimamisha nyota wawili wa timu hiyo kipa, Hussein Shariff 'Casillas' na beki, Erick Kyaruzi kwa kile kilichoelezwa kuihujumu.
Mabao ya Yanga katika mchezo huo yalifungwa na Obrey Chirwa na Donald Ngoma waliofunga mawili kila mmoja wao huku Simon Msuva na Deus Kaseke wakifunga moja moja wakati ya Kagera Sugar yalifungwa na Mbaraka Yusuph aliyefunga yote.
Yanga imeendeleza rekodi nzuri katika Ligi Kuu Bara inapocheza ikiwa uwanja wake wa nyumbani kwa sababu haijawahi kupoteza au kutoka sare tangu msimu huu wa 2023/2024 umeanza.
Huu unakuwa ni mchezo wa 13 kwa Yanga ikiwa mwenyeji na kati ya hiyo imeshinda yote sawa na kukusanya pointi 39 ambapo imefunga jumla ya mabao 33 na kuruhusu matano tu.
Kwa upande wa michezo mingine 13 iliyocheza ya ugenini Yanga msimu huu imeshinda tisa, sare miwili na kupoteza pia miwili ambapo kati ya hiyo imefunga mabao 24 na kuruhusu saba na kukusanya pointi zake 29.
Ushindi wa leo unaifanya Yanga kufikisha pointi 68 katika michezo 26 iliyocheza hivyo kuhitaji pointi tano tu ili kufikisha 73 zitakazowapa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya tatu mfululizo na wa 30 kwa ujumla tangu mwaka 1965 kwa sababu hazitaweza kufikiwa na timu yoyote.
Iko hivi, Azam FC inayoshika nafasi ya pili na pointi 57 hata ikishinda michezo yake yote mitano iliyobakia itafikisha pointi 72 huku kwa upande wa Simba inayoshika nafasi ya tatu na pointi 53 ikishinda mechi zake zote sita zilizobakia itamaliza msimu huu na pointi 71.
Kagera inafikisha michezo 26 ya Ligi Kuu Bara msimu huu ambapo kati ya hiyo imeshinda sita, sare 12 na kupoteza minane ikiwa nafasi ya saba na pointi 30.