Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga wakomba mamilioni ya Azam

YANGA DUBAI 1 1140x640 Kikosi cha Yanga

Tue, 28 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kikosi cha Yanga usiku wa juzi kilikuwa ugenini mjini Bamako, nchini Mali kupepetana na Real Bamako katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini vinara hao wa Ligi Kuu Bara, tayari imejihakikisha Sh200 milioni zikiwa kama bonasi kutoka Azam Media.

Ipo hivi. Yanga kwa sasa inahitaji ushindi kwenye mechi nne kati ya saba zijazo za ligi hiyo ili watangaze rasmi ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo, lakini kabla hata ya hizo mechi, tayari imewaacha kwenye mataa wapinzani wake Simba na Azam katika vita ya kuwania mamilioni ya fedha za udhamini wa haki za matangazo ya luninga.

Kwa pointi 62 ilizonazo kileleni kwa sasa imeifanya iongoze msimamo wa ligi, Yanga ndio timu pekee hadi sasa kwenye ligi ambayo imejihakikishia kumaliza katika nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi na hadi sasa ina uhakika wa kuvuna kiasi cha Sh200 milioni kutoka Kampuni ya Azam Media kama bonasi.

Yanga imesaliwa na mechi dhidi ya Geita Gold, Kagera Sugar, Simba, Singida Big Stars, Dodoma Jiji, Mbeya City na Tanzania Prisons na kama itashinda hizo nne za kwanza ikiwamo ya Simba iliyopangwa kupigwa Aprili 16 itatetea taji kabla ya ligi kufikia tamati Mei 28 mwaka huu.

Hata Yanga ikipoteza mechi zake zote saba zilizobakia kwenye ligi kuu msimu huu, ina uhakika wa kumaliza katika nafasi nne za juu kwani pointi zake 62 zitaweza kufikiwa na timu tatu tu ambazo ni Simba, Azam na Singida Big Stars.

Kwa mujibu wa mchanganuo wa bonasi katika udhamini wa Azam Media wa haki za matangazo za Ligi Kuu, timu inayochukua ubingwa, inapata bonasi ya Sh500 milioni, mshindi wa pili atapata Sh250 milioni, mshindi wa tatu atavuna Sh225 milioni na inayomaliza katika nafasi ya nne inapata Sh200 milioni. Ikiwa Yanga itavuna pointi nne katika mechi mbili zijazo, itakuwa na uhakika wa kuvuna Sh250 milioni na itabakia na kibarua kimoja tu ambacho ni kushinda mechi tatu zitakzofuata ili ijihakikishie ubingwa na Sh500 milioni.

Simba na Azam FC zenyewe hadi sasa bado hazijajihakikishia kumaliza katika nafasi nne za juu na hizo Sh200 milioni kwani pointi zilizonazo sasa zinaweza kufikiwa na kupitwa na Geita Gold.

Ili ijihakikishie kiasi hicho cha fedha, Simba inahitajika kushinda mechi moja tu, lakini ikishinda mechi nne zinazofuata itajihakikishia kitita cha nafasi ya pili cha Sh250 milioni kwani pointi zake hazitoweza kufikiwa na Azam, Singida Big Stars wala Geita Gold.

Kibarua kigumu kipo kwa Azam FC kwani pointi 47 ilizonazo, zinaweza kufikiwa na Geita Gold, Singida Big Stars, Kagera Sugar na Ihefu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live