Viongozi Klabu ya Yanga wameanza mapema kukifanyia maboresho kikosi chao kuelekea msimu ujao, baada ya kupiga hodi kuulizia huduma ya kiungo mkabaji, Yusuph Kagoma kama mbadala mpya wa staa wao, Khalid Aucho.
Kagoma ni kati ya viungo wakabaji wazawa wanaofanya vizuri katika Ligi Kuu ambapo msimu huu amekuwa akiitumikia Singida Fountain Gate aliyojiunga nayo kipindi cha usajili wa dirisha dogo msimu wa 2022/23 akitokea Geita Gold kwa mkataba wa miaka miwili.
Kiungo huyo amebakiwa na miezi sita kumaliza muda wake na hivi karibuni iliripotiwa kwamba ameondoka kambini huko Singida Fountain Gate kutokana na kilichoelezwa kudai stahiki zake ambapo mara ya mwisho kuonekana uwanjani akiitumikia timu hiyo ikiwa ni Machi 16, 2024 katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo.