Mabingwa watetezi, Yanga SC wameibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Coastal Unión katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.
Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, mshambuliaji Muivory Coast, Joseph Guede Gnadou dakika ya 76 akimalizia pasi ya Mzambia, Kennedy Musonda.
Coastal Union ilimaliza pungufu baada ya beki wake Lameck Lawi kutolewa kwa kadi nyekundu dakika 69 kufuatia kumvuta jezi kiungo Mburkinabe wa Yanga, Stephane Aziz Ki akiwa anakwenda kufunga.
Kwa ushindi huo, Yanga inafikisha pointi 64 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi nane zaidi ya Azam FC, wakati Coastal Unión inabaki na pointi zake 33 nafasi ya nne baada ya wote kucheza mechi 24. Vigogo wengine, Simba SC wapo nafasi ya tatu wakiwa na pointi 46 baada ya kucheza mechi 21.