Kiungo wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Athuman Idd ‘Chuji’ ameitahadharisha Yanga kuwa makini na mipira iliyokufa (frii-kiki na kona), katika mashindano ya kimataifa kwani imekuwa ikiwapa shida.
Yanga itacheza leo Jumatano kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam na Real Bamako ya Mali katika mechi ya kundi D ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika mchezo uliopita timu hizo zilitoka sare ya kufungana bao 1-1, mchezo uliofanyika nchini Mali huku bao la Bamako likiwa la kona ya dakika ya mwisho baada ya mabeki wa Yanga kushindwa kuokoa na kumpa nafasi Emile Kone kuweka mpira kambani kwa kichwa.
Timu ya US Monastir ya Tunisia inaongoza Kundi D ikiwa na pointi saba, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi nne, TP Mazembe inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tatu na Real Bamako ina pointi mbili.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chuji alisema ameifuatilia Yanga na kugundua ina changamoto katika mipira iliyokufa kwa baadhi ya wachezaji kushindwa kukabidhiana majukumu ya kukaba.
“Inapotokea frii-kiki au kona tuongeze umakini, kwenye mwamba aanze mchezaji wetu, mpira usipite, kubwa ni kukaba mtu kwa mtu bila kutegeana, hili la kukaa mbele ya mpira ni muhimu ili kumpoteza mpigaji.
“Tuna tatizo hilo na ni kubwa. Unaweza ukacheza vizuri lakini ikitokea friikiki unafungwa, inakuwa kazi bure. Ni muhimu sana Yanga ijipange. Ipo vizuri ila kwenye mipira iliyokufa kuna shida,” alisema
Chuji alisema Watanzania wote wapo nyuma ya timu hiyo hivyo wachezaji wasiwaangushe wacheze kwa kupambana ili kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri.
“Yanga sasa hivi timu ina rythim ya ushindi, wachezaji wanapambana, nakubali tumekuwa bora lakini tunatakiwa kuongeza jitihada zaidi, mashindano ya kimataifa ni magumu na yanahesabu nyingi unaweza ukacheza vizuri usipate matokeo mazuri.
“Wapo nyumbani, waitumie nyumbani kupata matokeo mazuri na sio jambo jingine kwa sababu mashabiki wanataka ushindi,” alisema Chuji
Alisema anaipa nafasi kubwa Yanga kushinda kwa kuwa ni timu nzuri yenye wachezaji wanaojua kupambana kwani hata ilipopoteza Tunisia sio kwamba ilizidiwa, ilitawala mchezo isipokuwa iliotewa kwa mabao mawili ya mipira iliyokufa.