Mchezo wa Yanga vs CR Belouizdad [Ligi ya Mabingwa Afrika] ni mgumu katika mazingira mengi sana, timu zote zina nafasi ya kufuzu Robo Fainali na zote zinahitaji kushinda mchezo huo.
Mchezo wa kwanza kule Algeria, Yanga ilicheza vizuri sana lakini Belouizdad ilicheza kimkakati kutafuta matokeo. Yanga ilitawala mchezo halafu Belouizdad ikashinda mechi.
Bila shaka Belouizdad watakuja na mkakati mwingine wa kucheza ugenini huku wakijua Yanga ndio mshindani wao kwenye nafasi ya kufuzu Robo Fainali. Kama watapata alama yoyote Dar itakuwa nafuu kwao kwa sababu mchezo wao wa mwisho wanamaliza nyumbani dhidi ya Medeama.
Yanga wanajua fika kwamba endapo watadondosha alama kwa Belouizdad uwezekano wa kufuzu hatua ya Robo Fainali unazidi kuwa finyu!
Ili Yanga ifuzu bila kuangalia matokeo ya timu nyingine inabidi ipate alama nne au sita kwenye mechi zake mbili zijazo dhidi ya Belouizdad na Al Ahly.
Kwa hiyo wananchi wanatakiwa kushinda kwanza nyumbani dhidi ya Belouizdad halafu waanze kupiga hesabu za mchezo wao wa mwisho ugenini dhidi ya Al Ahly.