Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga waendelea kujifua, watuma salam Mbeya

Yanga A0001 Yanga waendelea kujifua, watuma salam Mbeya

Sat, 10 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Jumapili hii ya Februari 11, 2024 kikosi cha timu ya Young Africans SC kikiwa na mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Tanzania Prisons, Meneja, Walter Harson amefunguka kila kitu kuihusu timu yetu.

Katika mahojiano aliyofanya jana, Harrison amezungumzia kuhusu hali ya kikosi, kurejea kwa Stephane Aziz Ki, kupona kwa Bakari Mwamnyeto na hali za majeruhi wawili, Ibrahim Bacca na Gift Fred.

Mbali na hayo, Harson ametoa ratiba ya safari ya kikosi hicho kuelekea Mbeya kwa ajili ya mchezo huo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

“Kikosi cha Young Africans leo (jana) kimeendelea na mazoezi kwa maana ya kuiweka miili sawa baada ya mechi ya jana dhidi ya Mashujaa kutoka pale Kigoma na kupata ushindi wa magoli 2-1, kila kitu kimeenda vizuri.

UWEPO WA AZIZ KI

“Kikosi kimechagizwa na urejeo wa kiungo wetu Stephane Aziz Ki ambaye amerejea kutoka kwenye majukumu ya timu ya taifa katika michuano ya AFCON pale nchini Ivory Coast akiwa na timu yake ya taifa ya Burkina Faso, amekuja kuongeza kitu kwenye timu na tunategemea ujio wake utaendelea kuimarisha kikosi chetu hasa kipindi hiki ambacho tunawakosa baadhi ya wachezaji ambao wamerejea wakiwa kwenye hali ambazo sio za utimamu wa miili kuelekea kwenye kumalizia raundi ya kwanza ya ligi na kuanza raundi ya pili.

KUHUSU SAFARI

“Kikosi kitasafiri kuelekea pale mkoani Mbeya kesho majira ya jioni saa 10 na dakika 45, baada ya kufika Mbeya, kitafanya mazoezi kidogo ya kuweka miili sawa kabla ya siku ya Jumapili kuweza kuingia dimbani dhidi ya Tanzania Prisons.

“Tunajua Tanzania Prisons ni timu nzuri, timu ambayo imekuwa ikionesha ushindani mkubwa kwenye ligi, lakini pindi ambapo inacheza pia na Young Africans, tunaelewa ugumu wa mchezo na umuhimu wake, tunategemea kwa kiasi kikubwa utakuwa ni mchezo mzuri ambao kila mmoja ataenda kuonesha uwezo wake.

“Tunaamini kuwa kwa kikosi tulichonacho tutakuwa kwenye mazingira mazuri ya kupata alama tatu na kuendelea kukaa katika kilele cha ligi na kuwapa zawadi nzuri sana Wananchi, zawadi ya birthday ya miaka 89 tangu kuzaliwa kwa Young Africans.

KUREJEA KWA MWAMNYETO

“Tunategemea urejeo wa Bakari Nondo Mwamnyeto katika kikosi baada ya kurejea akiwa na majeraha akitokea katika timu ya taifa kwenye michuano ya AFCON, hivyo anarejea katika kikosi na atakuwa kwenye safari.

HALI ZA MAJERUHI

“Tunategemea kuwakosa baadhi ya wachezaji ambao wanaweza wakawa wamepata majeraha kwenye mchezo wa jana na itategemea na ripoti ya daktari mpaka pale ambapo tutakuwa tunasafiri, kwa maana ya Ibrahim Abdullah (Bacca) pamoja na Gift Fred, hao ndio wachezaji ambao mpaka kesho muda wa kusafiri tutakuwa tumeshajua hali zao na kujua kama wataambatana na timu au la, lakini kwa wengine wote watakuwa tayari kuhakikisha wanakuwa sehemu ya kikosi cha Young Africans ambacho kitaelekea pale Mbeya kwenda kuwavaa Tanzania Prisons.

OMBI KWA WANANCHI

“Kikubwa tunaomba mashabiki wetu wajitokeze na kama ambavyo itakuwa siku ya kilele cha miaka 89, tunaamini nguvu yao itakuja kusheresha siku hii muhimu kwetu ambayo kiuhalisia tunahitaji zaidi pointi tatu ili kuweza kuhakikisha tunasherehekea birthday hii ya Wananchi,” alisema Harrison.

Ikumbukwe kwamba, siku ya mchezo huo, ndio itakuwa kilele cha kuadhimisha miaka 89 tangu kuanzishwa kwa Klabu ya Young Africans mwaka 1935.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live