Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga vs Simba: Ni vita ya mtu na mtu

Inonga Mayele Yanga na Simba watakutana Jumamosi hii April 30 katika Uwanja

Thu, 28 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Jumamosi Jioni Tanzania itasimama kwa muda. Simba na Yanga zitakuwa na jambo lao kwenye Uwanja wa Mkapa katika mechi ngumu ya watani wa jadi.

Ni mechi gumzo ambayo licha ya matokeo yake kubeba heshima ya mtani lakini pointi tatu ni muhimu vilevile kwenye mbio za ubingwa msimu huu.

Wakati mambo yakizidi kunoga nje ya uwanja kuna vita nyingine itakuwa ndani ya Uwanja ambapo kutakuwa na mapambano mengine tisa ya kibabe kati ya mtu na mtu kila mmoja akitaka kumtuliza mwenzake na kuweka heshima mjini;

Mayele vs Inonga

Kinara wa mabao ndani ya kikosi cha Yanga ni mshambuliaji Fiston Mayele ambaye amefunga mabao 12 lakini Mkongomani huyu atakuwa na vita na Mkongomani mwenzake Inonga Baka wa Simba ambao katika pambano la kwanza walipambana na beki huyo kuonyesha amemdhibiti na sasa mwenzake anataka kuja kulipa kisasi. Ni mabesti wakubwa nje ya Uwanja lakini hata nchini kwao kila mmoja hutaka kupata sifa zaidi kupitia mechi hii.

Chama vs Bangala

Kiungo Clatous Chama amerejea nchini na pambano lake la kwanza la watani litakuwa hili hakuna namna lazima Mzambia huyu awe uwanjani na hapa atakuwa na kazi nzito na kiungo Yannick Bangala ambaye anaweza kukabidhiwa mtu huyo asifanye balaa lake. Wote wawili ni mafundi wakubwa wa mpira na wanaheshimika zaidi na mashabiki wao kutokana na ukongwe na ubora.

Mkude vs Feisal

Kiungo cha ukabaji kwa Simba kitakuwa chini ya Jonas Mkude ambaye atakuwa na hasira baada ya kukosa penalti timu yake ikitupwa nje hapa atakuwa na kazi ya kumzuia Feisal Salum ‘Fei toto ambaye amerejea na moto wake wa mabao baada ya kufunga katika mchezo uliopita. Ni wachezaji wazawa ambao wameizoea mechi hii na hawanaga mchecheto.

Diara vs Manula

Pambano lingine litakuwa kwa makipa Aishi Manula wa Simba ambaye kwa msimu huu amesharuhusu mabao saba kwenye ligi akichuana na kipa chaguo la kwanza wa Yanga Diara Djigui ambaye ameruhusu mabao 6 mpaka sasa na utamu wa hawa jamaa ni kwamba mmoja akifungwa mechi hii mwingine naye anafungwa kule je, nani atatoka salama? Jumamosi jioni tutapata wakati tunafuturu.

Morrison vs Djuma

Hapa pana kazi. Winga machachari dhidi ya beki machachari. Bernard Morrison wa Simba atakuwa katika vita kubwa na beki wa kulia wa Yanga Djuma Shaban, kumbuka ubora wa Morrison uko juu kwasasa na Djuma naye hajawahi kuchuja. Sasa hapa ndipo viwango vitazungumza.

Tshabalala vs Moloko

Winga wa Yanga, Jesus Moloko amerejea kazini na huenda akarudishiwa namba yake ya winga wa kulia na hapa atakuwa na kazi na nahodha msaidizi wa Simba beki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye yuko katika kiwango bora kwasasa. Ni eneo ambao litakuwa na ufundi wa namna yake kwani wachezaji hawa wanajuana vizuri.

Saido vs Kapombe

Beki wa kulia wa Simba Shomari Kapombe naye yuko katika kiwango bora sana kwasasa lakini kazi yake itakuwa kumzuia mkongwe Said Ntibazonkiza ‘Saido’ ambaye ana nafasi kubwa ya kuanza kwenye mchezo huu.

Mwamnyeto vs Mugalu

Simba wanaweza kumtanguliza mshambuliaji wao Chriss Mugalu ambaye amekuwa akiaminiwa na benchi la ufundi la timu hiyo,Mugalu hapa atakuwa chini ya ulinzi wa beki na nahodha wa Yanga Bakari Mwamnyeto. Acha wamalizane.

Sakho vs Kibwana

Simba staa wao mwingine ambaye watategemea kazi yake bora ni mshambuliaji Pape Sakho ambaye anajua kusumbua na mara nyingi akitokea kushoto na kuingia ndani hapa atakuwa na vita na beki wa kushoto wa Yanga Kibwana Shomari ambaye anaaminika kwa hesabu kali.

Kaze vs Pablo

Hapa kwa makocha na penyewe pamoto. Simba itakuwa chini ya Pablo Franco ambaye atakuwa anaiongoza Simba katika mechi ya pili akitangulia kupata suluhu vita yake itakuwa na kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze kwani Mohammed Nabi anatumikia adhabu. Kaze hajawahi kuifunga Simba kwenye ligi, nani atamkimbia mwenzake. Jumamosi jioni tutajua.

LAKINI KUNA MAMBO HAYA

Kuongoza Ligi

Mpaka inaingia kwenye mchezo huo Yanga itakuwa ipo juu ya msimamo wakiongoza wakiwa na pointi 54 baada ya kucheza michezo 20 na balaa la Yanga ni kwamba tangu wapande hapo baada ya mechi tatu tu yaani kuanzia Oktoba 27,2021 hawajashuka hapo.

Simba imeendelea kushika nafasi ya pili wakiwa na pointi 41 baada ya kucheza michezo 19 na sasa wanatofautiana na Yanga kwa jumla ya pointi 13 ingawa wekundu hao wana mchezo mmoja pungufu mkononi na hata kama wakicheza na kushinda tofauti itabaki kuwa pointi 10.

Kapoteza, Hajapoteza

Yanga mpaka sasa haijapoteza kwenye ligi na matokeo yao mabaya yamekuwa ni sare 3 ambazo mbili kati ya hizo ni ile moja ambayo walitoka suluhu dhidi ya Simba katika mzunguko wa kwanza ‘Wananchi’ wakionekana kuwa katika ubora mkubwa.

Simba wao wako katika msimu wa hesabu kali na mpaka wanakutana na Yanga walishapoteza mechi ambazo ziliwashtua wakitangulia kufungwa na Mbeya City kisha wakafuata kutibuliwa na Kagera Sugar mechi zote wakipoteza kwa bao 1-0.

Yanga imefunga mengi

Eneo lingine la ubora ni kwamba Yanga inaonekana kuwa na safu bora ya ushambuliaji wakifunga jumla ya mabao 35 lakini eneo lingine wanaonekana kuwa na ukuta mgumu wakiruhusu mabao 6 pekee katika mechi zao hizo.

Simba wamefunga 23, wakaruhusu 7

Simba wao wako tofauti kidogo hapa nako wanaonekana kuwa na unyonge wakifunga mabao 23 ikiwa na tofautu na misimu minne iliyopita huku pia ukuta wao ukiruhusu jumla ya mabao 7 mpaka sasa.

Yanga Mayele, Simba Kagere

Mabeki wa Simba kama kuna mshambuliaji watataka kumzuia ni Fiston Mayele jamaa anaonekana kuwa katika moto mkali wa kufunga akiwa ameshafunga mabao 12 kwenye ligi akiongoza katika msimamo wa wafungaji na kibaya zaidi Mkongomani huyo amefunga katika kila mechi zake sita zilizopita wakati anakwenda kukutana na Simba akiwa hajazifunga timu mbili pekee Simba na Mbeya City.

Simba wao kinara wao wa mabao mpaka sasa ni Meddie Kagere ambaye amefunga mabao 7 katika mechi ambazo amecheza ikiwa ni anguko kubwa la Simba katika miaka ya karibuni.

Nabi, Pablo

Yanga kocha wao Nasreddine Nabi mpaka sasa ameshachukua tuzo mbili za kuwa kocha bora wa mwezi katika miezi ya Oktoba na Februari akiwa ndio kocha pekee aliyechukua tuzo hizo mara mbili mpaka sasa msimu huu wakati kocha wa Simba Pablo Franco yeye akichukua tuzo hiyo mara moja mwezi Machi.

Makocha hao wamegongana eneo moja kwamba wote wamewahi kusimamishwa kwa makosa ya utovu wa nidhamu, Nabi hatakuwa katika benchi la Yanga katika mchezo huu baada ya kusimamishwa hivi karibuni lakini Pablo naye aliwahi kukumbana na adhabu kama hii kwa makosa kama hayo.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz