Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga vs Pyramids: Mwarabu anapigwa hivi!

79837 Pyramid+pic

Tue, 15 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

YANGA itaikaribisha Pyramids ya Misri katika mechi ya kwanza ya mchujo wa kuwania kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Mchezo huo utapigwa Uwanja wa Taifa, Oktoba 27 kisha kurudiana Novemba 3.

Kikosi cha Pyramids kuundwa na wachezaji wenye thamani ya Sh. 52 bilioni wakiwamo nyota saba wa timu ya Taifa ya Misri, kimezua mjadala mzito kwamba Yanga tayari imeaga mashindano huku wengine wakitania kwamba, ni bora ijitoe yenyewe tu.

Lakini soka haliko hivyo. Ni lazima mpira uchezwe. Na kuna mifano mingi ya vikosi vya thamani ndogo vilivyodhalilisha timu kubwa zenye vikosi vya bei mbaya kama Real Madrid ilivyotolewa dhidi ya Ajax katika Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita na mifano mingine mingi.

Hapa Mwanaspoti linakuchambulia mambo yanayoweza kuibeba Yanga kushinda kiulaini.

Uimara wa Yanga

Eneo ambalo Yanga imekuwa imara kwa sasa ni matumizi mazuri ya mipira ya faulo, kona na penati na imekuwa na idadi kubwa ya wachezaji ambao, wamekuwa wakiimudu vilivyo katika kuwamaliza wapinzani.

Pia Soma

Advertisement
Mabao mengi ambayo Yanga imefunga msimu huu yametokana na aina hiyo ya mipira na sio nafasi za kawaida ambazo imekuwa ikitengeneza.

Kama Yanga watajiimarisha zaidi eneo hilo, lakini pia kutumia nafasi za kawaida na kuongeza kasi waliyonayo, wanapata ushindi mnono.

Pia, Yanga inabebwa na uzoefu walionao katika mashindano ya kimataifa kulinganisha na wapinzani wao na jambo hilo linaiweka kwenye hali nzuri kisaikolojia kushinda dhidi ya wapinzani wao hao.

Wakati Pyramids wakiwa hawana historia wanayoweza kuitambia, Yanga imetinga hatua ya makundi kwenye mashindano ya klabu Afrika mara tatu tofauti na moja ni Ligi ya Mabingwa Afrika na mara mbili Shirikisho.

Kinachowapa jeuri zaidi Yanga, mara mbili ambazo walitinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, walipenya kupitia mechi za mchujo kama hizi ambapo, mwaka 2016 waliingia baada ya kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola na mwaka 2018 waliitupa nje Welayta Dicha ya Ethiopia.

Pia, mara zote ambazo Yanga ilitinga hatua ya makundi ya Shirikisho, ilifanya hivyo baada ya kuondolewa Ligi ya Mabingwa Afrika. Lakini, kitendo cha Pyramids kutowafahamu vyema kinaipa faida Yanga kwani, itawalazimu Waarabu hao kuwasoma kupitia mechi itakayowakutanisha na hivyo, Yanga inaweza kutumia mwanya huo kuwamaliza mapema sana.

Udhaifu Yanga

Miongoni mwa kasoro zinazoitesa Yanga ni kikosi chake kukosa muunganiko mzuri ndani ya uwanja, ambapo kwa sasa kinaonekana kutegemea zaidi juhudi na uwezo wa mchezaji mmojammoja na sio kitimu.

Kukosekana huko kwa muunganiko wa kitimu kumeifanya Yanga ikose balansi katika kushambulia, kumiliki mpira na jambo ambalo limekuwa likiifanya iwe na wakati mgumu pindi inaposhambuliwa, ishindwe kupata mabao na hata kuzidiwa katika kutawala mchezo.

Ukiondoa hiyo, kingine ni kukosa umakini na utulivu katika safu ya ushambuliaji kutumia vyema nafasi za kufunga wanapokuwa langoni mwa adui.

Hilo limeifanya Yanga ipoteze nafasi inazotengeneza na kujikuta ikifunga idadi ndogo ya mabao ambayo kwa asilimia kubwa yanatokana na mipira ya adhabu ndogo, kona na penati badala yale ya yale ya muvi.

Lakini, pia udhaifu wa safu ya ulinzi hasa kukosa mawasiliano umeifanya Yanga kujikuta ikifanya makosa ya mara kwa mara katika safu yake ya ulinzi hivyo, kuruhusu mabao kizembe.

Kasoro nyingine kwa Yanga ni upangaji usio sahihi wa kikosi kwa kuwapa nafasi wachezaji ambao, hawatoi mchango mkubwa kwa timu, lakini pia kupanga wachezaji kwenye nafasi tofauti na zile ambazo wamezoea kucheza jambo ambalo limewafanya wawe na ufanisi duni kikosini.

Mfano katika baadhi ya mechi, beki wa kati, Ally Ally amekuwa akipangwa kama beki wa kulia vivyo hivyo kwa mlinzi mwingine Seleman Mustafa au kiungo Mapinduzi Balama wakati huo mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kufumania nyavu, Juma Balinya akiwa anasubiri benchi ama kutotumika.

Hata hivyo, changamoto ya majeruhi ni eneo lingine ambalo linaiangusha Yanga ambayo imejikuta ikiwa na kikosi kidogo hivyo kulinyima wigo mpana wa uteuzi benchi lake la ufundi, lakini pia itamkosa beki Lamine Moro anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu hivyo, atakosa mechi ya kwanza ya Pyramids.

Yanga ifanye nini

Soka la kasi kwa safu ya ushambuliaji linaweza kuwa silaha muhimu kwa Yanga kupata matokeo kwenye mchezo huo.

Pamoja na makali iliyonayo safu hiyo, safu ya ulinzi ya Pyramids FC imekuwa na udhaifu wa kufanya makosa yatokanayo na kushindwa kuhimili presha ya mashambulizi ya timu pinzani na kujikuta ikiruhusu mabao.

Lakini, pia Yanga inapaswa kuhakikisha wachezaji wake hawapotezi mpira mara kwa mara kwenda kwa adui kwani, timu hiyo ni hodari na wana uwezo wa hali ya juu wa kushambulia na kufanya uamuzi wa haraka wanaponasa mpira kwa adui.

Wachezaji watakaocheza nafasi za pembeni upande wa Yanga kwa maana ya mabeki wa kulia na kushoto pamoja na mawinga wanapaswa kucheza kwa tahadhari kubwa na wawe na pumzi na stamina ya kutosha ili kuwadhibiti wachezaji wa pembeni wa Pyramids FC hasa wale wa kulia.

Mashambulizi mengi ya Pyramids FC huanzia pembeni na kupigwa krosi na hayo ndio yanachangia kupatikana kwa mabao. Lakini, upangaji mzuri wa kikosi na mbinu unaweza kuwa silaha ya kuibeba Yanga mbele kwenye mechi hizo vinginevyo inaweza kukwama.

Kimbinu, Pyramids FC inatumia zaidi mfumo wa 4-1-4-1 ambao una viungo watano na kati yao wanne hushambulia huku mmoja akisaidia jukumu la ulinzi. Lakini, katika viungo hao wanne wa kushambulia timu hiyo huanza na kiungo mmoja tu asilia wa kushambulia huku mawinga watatu ambao wawili wanacheza kulia na kushoto kila mmoja kisha kuna winga mwingine, ambaye anakuwa huru kuzunguka maeneo tofauti uwanjani.

Kwa maana hiyo ni lazima Yanga iwe imara zaidi katika kiungo hasa ya ulinzi na itafaa zaidi kama itaanza na viungo wawili wakabaji wataokuwa na kazi ya kutibua mbinu za viungo washambuliaji wa Pyramids FC.

Mambo mengine mawili ambayo yanaweza kuwa chachu kwa Yanga kupata ushindi ni kuimarisha ufanisi katika kushambulia na kuwaandaa vyema kisaikolojia wachezaji wake. Wachezaji hawapaswi kuingia na presha kwani, wanaweza kukosa utulivu na kumpa faida adui.

Pia, Yanga inapaswa kuwa na idadi kubwa ya wachezaji kwenye eneo la hatari la adui pindi inaposhambulia kwani, uwepo wa namba ndogo imekuwa ikiwapa kazi nyepesi wapinzani kuondoa hatari.

WASIKIE HAWA

Katika kujiweka fiti kabla ya kuivaa Pyramids FC, Yanga imepanga kucheza mechi mbili za kirafiki na Friends Rangers na Pan African za Daraja la Kwanza ikiamini ni kipimo kizuri.

Hata hivyo, kumekuwa na mitazamo tofauti kwa wadau wa soka juu ya uamuzi huo wa kucheza na timu hizo kama sehemu ya maandalizi.

“Kiuhalisia na kiufundi mechi hizi hazina msaada kwa Yanga. Wakiwa katika maandalizi ya msimu, walicheza dhidi ya timu za aina hiyo na kuzifunga idadi kubwa ya mabao jambo ambalo linaonekana liliwaathiri kisaikolojia wachezaji wakaona kwamba, wamekamilika na timu iko vizuri lakini mambo yamekuwa tofauti kabisa katika mechi za mashindano.

“Tukumbuke hizo ni timu za Ligi Daraja la Kwanza ambazo malengo na mbinu zao ni kwa ajili ya kupanda daraja hivyo, haziwezi kuwa na ubora wa kuipa Yanga kile inachokihitaji. Kama zingekuwa na ubora basi zingekuwepo Ligi Kuu Bara.

“Inawezekana wamefanya hivyo wakiamini kuwa watazitumia mechi hizo kufanya tathmini ya namna gani wachezaji wamekipokea kwenye maandalizi, lakini tathmini hiyo haiwezi kuwa sahihi,” alisema mchambuzi wa soka wa Mwanaspoti, Mwalimu Alex Kashasha.

Naye aliyewahi kuwa kocha wa Yanga, Kenny Mwaisabula amesema mchezo huo unatakiwa kumalizwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kwa Yanga kufunga mabao ya kutosha kisha kutafuta sare katika mechi ya marudiano kule Misri.

“Wale waarabu ni wazuri sana wanapokuwa ugenini na kupoteza huwa nadra hivyo, Yanga wana kazi kubwa ya kumaliza mchezo nyumbani. Lazima wafunge mabao ya kutosha ili kutanguliuza mguu mmoja ndani kisha kwenda kukomaa,” alisema Mwaisabula.

Zahera: MSIOGOPE KIKOSI, TUNAJIPANGA

Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema anawaheshimu Pyramids FC, lakini kamwe haogopi ukubwa wa kikosi walichonacho kwa kuwa, ameshughudia timu ndogo ikizifunga timu zenye vikosi vya gharama kubwa.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa simu, Zahera, ambaye kwa sasa yuko kambini na timu ya Taifa ya DR Congo, amesema mashabiki wasitishwe na ukubwa wa kikosi cha wapinzani wao na kwamba, dakika 90 ndio zitaamua nani ataondoka na ushindi kwenye mechi hiyo.

“Dadika 90 ndio zitaamua nani ni bora, kikubwa ni kujiandaa vyema kuwakabili wapinzani wetu ambao hawana uzoefu wa mashindano haya kama ilivyo kwetu,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz