Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga vs KMC safari ya ubingwa, kubaki TPL

98800 Yanga+pic Yanga vs KMC safari ya ubingwa, kubaki TPL

Fri, 13 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Simba, Yanga leo ina kibarua cha kuendeleza pale ilipoishia itakapoikabili KMC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara (TPL) katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Ushindi dhidi ya KMC ndilo jambo pekee ambalo litawafanya Yanga kuendelea kubaki na matumaini ya kufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu ambao hata hivyo wana nafasi finyu ya kutimiza ndoto hiyo.

Matokeo hayo yatawafanya wafikishe pointi 53 na kuendelea kuifukuzia Simba iliyopo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ambapo ina pointi 71.

Kiwango bora walichoonyesha Yanga dhidi ya Simba katika mchezo ambao waliibuka na ushindi wa bao 1-0 Jumamosi iliyopita kinatazamiwa kuwa mlima mrefu kwa KMC ikiwa tu wapinzani wao watakuwa vizuri katika mchezo wa leo, vinginevyo wanaweza kujikuta wakiambulia kipigo.

KMC pamoja na kuwa na mwendo wa kusuasua msimu huu ikikamata nafasi ya 18 katika msimamo wa ligi na pointi zake 27, sio timu ya kubeza na imekuwa ikionyesha ushindani wa hali ya juu katika mechi zake ambazo imekuwa ikicheza na timu zilizo juu ya msimamo wa ligi.

Wakati kwa Yanga hesabu zao kubwa ni namna gani wataibuka na ushindi leo ili angalau waendelee kuwa na uwezekano wa kupambana na Simba katika mbio za ubingwa, hali ni tofauti kwa KMC ambayo ushindi utafufua matumaini yao ya kubaki Ligi Kuu.

Pia Soma

Advertisement
Changamoto ya majeruhi ndio inaonekana kuiathiri zaidi timu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na huenda leo ikaendelea kuwakosa baadhi ya nyota wake kutokana na majeraha.

Wachezaji hao wengi ni wale wanaocheza katika safu ya ulinzi kama Abdallah Mfuko na Baptiste Mugiraneza.

Hata hivyo, mechi hiyo inaonekana itatawaliwa zaidi katika eneo la kiungo kutokana na timu zote mbili kuwa na mazoea ya kujaza idadi kubwa ya wachezaji katika sehemu hiyo.

Kwa Yanga, yenyewe ipo kwenye hatihati ya kumtumia nyota wake tegemeo, Bernard Morrison ambaye bado hajawa fiti kwa asilimia 100 baada ya kupata majeraha katika mchezo dhidi ya Simba ambao waliibuka na ushindi wa bao 1-0 alilofunga yeye mwenyewe.

Kocha wa KMC, Haruna Harerimana alisema kuwa vijana wake wamejipanga vyema kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mchezo huo.

“Tunaiheshimu Yanga kwani ni timu kubwa na imekuwa ikifanya vizuri na juzi imetoka kupata ushindi dhidi ya Simba, lakini tumejiandaa vyema kimbinu kuwakabili,” alisema.

“Ni lazima wachezaji wangu wawe na nidhamu ya hali ya juu ya mbinu na watumie vyema nafasi za mabao tutakazopata.”

Kwa upande wake, kocha wa Yanga, Luc Eymael alisema hawawezi kuidharau KMC, bali wanaipa uzito mkubwa mechi hiyo. “Matokeo ya mechi dhidi ya Simba yameshapita na sasa akili yetu ipo kwa KMC. Naamini mchezo utakuwa ni wa ushindani kwani wapinzani wetu wamekuwa wakitumia mbinu ya kushambulia kwa kushtukiza, hivyo tunapaswa kucheza kwa umakini wa hali ya juu,” alisema Eymael.

Chanzo: mwananchi.co.tz