Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga vs Ihefu mechi ya kisasi, kazi ipo hapa

Yanga X Ihefu Yanga vs Ihefu mechi ya kisasi, kazi ipo hapa

Mon, 11 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ukisikia mechi ya kisasi ndo hii. Kikosi cha Yanga kikiwa na rekodi tamu ya kushinda mechi tano mfululizo za Ligi Kuu Bara, jioni ya leo Jumatatu kinarejea tena uwanjani kukabiliana na Ihefu FC, timu pekee iliyowatungua msimu huu.

Mechi hiyo pekee kwa leo itapigwa kuanzia saa 12:00 jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex ambao wenyeji hawajapoteza katika michezo minane iliyocheza hapo msimu huu, lakini ikiwa na kiu ya kutaka kulipa kisasi cha kipigo ilichopewa na wageni wao katika mechi ya duru la kwanza msimu huu.

Ihefu iliitungua Yanga kwa mabao 2-1 katika mechi hiyo ya kwanza iliyopigwa Oktoba 4, mwaka jana kwenye Uwanja wa Highland Estate, Mbarali Mbeya kikiwa ndicho kipigo pekee alichokutana nacho Kocha Miguel Gamondi katika Ligi Kuu tangu ajiunge na timu hiyo.

Hicho kilikuwa ni kipigo cha pili mfululizo kwa Yanga ikivaana na Ihefu jijini Mbeya, kwani ndio waliomtibulia pia, Kocha Nasreddine Nabi aliyekuwa akiinoa timu hiyo ya Jangwani kwa kucheza mechi 49 mfululizo bila kupoteza na kukutana na kipigo cha 2-1 kilichohitimisha ubabe huo, japo timu hiyo haijawahi kuishinda Yanga ikiwa jijini Dar.

Takwimu zinaonyesha katika mechi tano ilizopita kwa timu hiyzo zilipokutana katika Ligi tangu mwaka 2020, Ihefu imeshinda mbili za nyumbani na kupoteza moja ilipofumuliwa 3-0, huku ikipoteza michezo miwili ya ugenini, kitu ambacho huenda leo ikaikabili Yanga ili kutaka kulivua joho la unyonge mbele ya wenyeji wao hao wanaongoza ligi.

Yanga ikiendelea kukosa huduma za baadhi ya nyota tegemeo akiwamo kiungo Khalid Aucho, itaikabili Ihefu likiwa ni pambano la 18 kwao msimu huu na la tisa ikiwa nyumbani, huku ikitaka kuendeleza rekodi yao ya kushinda mfululizo tangu kurejea kwa ligi iliyokuwa imesimama karibu miezi miwili kupisha Kombe la Mapinduzi 2024 na Afcon 2023.

Ligi ilirejea Februari 2 na Yanga imecheza mechi sita, ikishinda tano mfululizo na moja ya kwanza ikilazimishwa suluhu ugenini na Kagera Sugar na mchezo wa mwisho imetoka kuifumua Namungo kwa mabao 3-1 mjini Lindi, wakati Ihefu katika mchezo wa mwisho ilipata ushindi nyumbani dhidi ya KMC iliyokuwa uwanjani jana kuikabili Tabora United.

Tofauti na Yanga iliyoshinda mechi zote tano zilizopita, kwa upande wa Ihefu inayowategemea nyota wapya waliotua kupitia dirisha dogo kutoka Singida FG, kama Elvis Rupia, Duke Abuya, Marouf Tchakei, Joash Onyango na kipa Abubakar Khomeiny, yenyewe imeshinda mechi tatu, ikapoteza moja na nyingine ilitoka sare nyumbani na Mashujaa.

Ihefu ilirejea kwenye ligi ikishinda 3-2 mbele ya Mtibwa, kisha ikainyuka Geita 2-1 kabla ya kupoteza 2-1 kwa Kagera Sugar, mechi zote zikipigwa ugenini, ndipo ikatoka sare ya 1-1 na Mashujaa na kuichapa KMC 1-0 ikiwa nyumbani na leo inarudi kuikabili Yanga huku ikiwa na rekodi isiyovutia kwa mechi hizo za ugenini.

Katika michezo 10 ya ugenini Ihefu, imeshinda mara mbili tu na nyingine kama hizo ikitoka sare, huku sita ikipasuka ikifunga mabao 10 na kuruhusu nyavu zao kuguswa mara 16 na kuvuna pointi nane kati ya 30 ilizopaswa kubeba kupitia mechi hizo.

KAZI IPO HAPA

Licha ya kuwa ni mechi ya kisasi baina ya timu hiyo, Yanga ikitaka kulipa kipigo ilichopewa duru la kwanza na Ihefu ikitaka kufuta unyonge wa ugenini mbele ya wababe hao wa Bara, lakini mechi hiyo itakuwa na vita nyingine ya nyota wa timu hizo.

Mabeki wa timu zote watakuwa na kibarua za kuwazuia washambuliaji wa timu pinzani kutokana na kasi nzuri ya kutupia nyavuni.

Mabeki wa Yanga wakiongozwa na nahodha Bakar Mwamnyeto, Ibrahim Bacca, Dickson Job, Nickson Kibabage na Yao Kouassi watakuwa na kazi wa kuwachunga kina Rupia, Abuya, Tchakei na wengine wakimtungue kipa atakayeanza langoni, japo ukuta huo unaonekana ni mgumu kwani katika mechi tano zilizopita imeruhusu mabao mawili tu.

Hata hivyo, kwa namna safu ya ushambuliaji wa Ihefu ikiongozwa na Tchakei na Rupia ilivyoweka rekodi ya kufunga walau bao moja kwenye kila mchezo kati ya mitano iliyocheza inawafanya kina Bacca kuwa makini.

Ihefu kupitia mechi tano zilizopita za Ligi Kuu, imefunga mabao manane, japo ukuta wao umeruhusu mabao sita kitu kinachoweza kuwa msala kwao wanapokutana na safu kali ya ushambuliaji ya Yanga inayoongozwa na Mudathir Yanga aliyefunga mabao matano katika mechi tano zilizopita ikiwa na wastani ya kufunga bao moja kila mchezo.

Pia kuna nyota wengine tishio eneo la ushambuliaji akiwamo Clement Mzize na kinara wa mabao wa timu hiyo, Stephane Aziz KI mwenye mabao 11, moja pungufu na aliyonayo Feisal Salum ‘Fei Toto’ anayeongoza orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu hadi sasa.

Mabeki wa Ihefu wakiongozwa na Onyango, Benson Mangolo, Faria Odongo na Benjamin Tanimu au Lenny Kissu aliyeitungua Yanga kwenye mechi zote za jijini Mbeya zilizopita watakuwa na kazi ya kuwazuia nyota wa Yanga wasiendelee moto wa kugawa vipigo vinono kama ilivyofanywa na timu nyingine ilizokutana nazo Chamazi.

MBIO ZA UBINGWA

Yanga inahitaji ushindi leo ili kuzidi kupanua pengo la pointi baina yao na Azam iliyopo nafasi ya pili na kwa watani wao Simba iliyowazidi pointi saba hadi sasa.

Yanga inaongoza msimamo ikiwa na pointi 46 baada ya mechi saba na kama itashinda itafikisha 49, kwani Azam ina pointi 44 kwa sasa lakini ikicheza michezo 20, wakati Simba yenye 39 imecheza mechi 17 na kesho itarudi uwanjani kukabiliana na Singida FG katika mfululizo wa michezo wa ligi hiyo iliyoingia raundi ya 21 kwa sasa.

Yanga inasaka taji la tatu mfululizo baada ya kulibeba mara mbili ikiwa na Nabi ikiwamo ile ya kutwaa bila kupoteza mechi yoyote kabla ya msimu uliopita kutibuliwa na Ihefu na Simba, lakini ikatetea taji.

Wababe hao wanajua kufanya uzembe mbele ya Ihefu itatoa nafasi kwa wanaochuana nao kwenye ubingwa kuwakaribia, mbaya ni kuna mechi moja ijayo kabla ya kucheza na Azam katika pambano linalosubiriwa kwa hamu kutokana na upinzani na ushindani uliopo baina ya timu hizo kwa siku za karibuni.

Kwa upande wa Ihefu matokeo mazuri kwao itawatoa katika nafasi ya nane hadi kuingia Sita Bora (kutegemea na matokeo ya mechi ya jana kati ya KMC yenye pointi 25 iliyokuwa ikivaana na Tabora United), kwani itaifanya ifikishe pointi 26. Kwa sasa ina 23 kupitia mechi 19 ilizocheza na kocha wa timu hiyo, Mecky Maxime amekiri hiyo ni mechi ngumu kutokana na kasi ya Yanga, lakini ameandaa timu ili kupata matokeo mazuri ugenini.

Maxime aliyetua katika timu hiyo baada ya kutemeshwa kibarua Kagera Sugar, anaamini Yanga inafungika hata ikiwa kwao, kitu cha muhimu ni wachezaji kujituma na kupambana kwa dakika zote 90.

Kocha huyo aliwahi kuifumua Yanga kwa mabao 3-0 wakati akiwa na Kagera Sugar katika mechi ilipoigwa Januari 15 mwaka 2020 wakati wababe hao wakimkaribisha kocha mkuu mpya, Luc Eymael, hivyo njia alizotumia kuwatia aibu Yanga Kwa Mkapa anaweza pia kuzitumia kwenye pambano la leo.

Kwa upande wa Gamondi, akizungumzia mchezo huo wa leo alikaririwa akisema; “Kwetu kila mechi ni muhimu na tunataka kushinda hivyo leo (jana) tunakwenda kufanya mazoezi ya mwisho ili kuwapa furaha Wananchi. Tunajua Ihefu ndio timu pekee iliyotujeruhi msimu huu na kesho (leo) ni siku nzuri ya kulipiza kisasi hiki, wachezaji wanafahamu, benchi la ufundi tunafahamu na tunaamini tutapata alama tatu.”

Kocha huyo raia wa Argentina aliongeza kwa kusema; “Binafsi sikufurahi kabisa tulivyocheza mchezo wetu dhidi ya Ihefu najua pia Wananchi hawakufurahi, hivyo nawaomba kesho (leo) wajitokeze kwa wingi kwa kuwa wachezaji wanatambua wao ndio mchezaji wa 12, waje kwa wingi kushuhudia burudani nzuri na tukipamba kupata alama tatu muhimu.”

VIKOSI TARAJIWA

Katika mchezo huo wa leo, huenda timu zote zisiwe na mabadiliko makubwa ya vikosi kulinganisha na vile vilivyocheza mechi zilizopita za timu hizo.

Kwa upande wa Yanga, huenda kukawa na mabadiliko langoni kwa Metacha Mnata kuanzia benchi, lakini maeneo mengine yanaweza kusalia kama ilivyocheza dhidi ya Namungo na kushinda mabao 3-1 kwa maana Yao Kouassi na Nickson Kibabage kucheza pembeni, huku Dickson Job na Ibrahim Bacca kusimama beki ya kati.

Eneo la kiungo hadi mbele kutakuwa na Salum Abubakar, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Clement Mzize, Stephane Aziz KI na Augustine Okrah wataliamsha, huku kwa upande wa Ihefu langoni anatarajiwa kusimama tena Abubakar Khomeny, huku Faria Odongo na Benson Mangolo wakicheza pembeni na kati atasimama mzee mzima, Joash Onyango na Benjamin Tanimu kama sio Lenny Kissu.

Kwa upande wa eneo la mbele Amande Momade, Hernest Malonga, Emmanuel Lobota, Elvis Rupia, Marouf Tchakei na Duke Abuya watalianzisha kama kawaida ili kuhakikisha mambo yanaenda vyema kwa timu hiyo iliyohamishia maskani yake kwa sasa mjini Singida kutoka jijini Mbeya.

Chanzo: Mwanaspoti