Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga vs Azam, vita ya kugombea nafasi kileleni

Azam Vs Yanga Mkwakwani Yanga vs Azam, vita ya kugombea nafasi kileleni

Mon, 23 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ligi Kuu Bara inaendelea leo kwa mchezo mmoja kupigwa ambapo macho na masikio ya mashabiki wa soka nchini yataelekezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa wakati Yanga itakapokuwa inaikaribisha matajiri wa jiji la Dar es Salaam, Azam FC.

Mchezo huu utakaopigwa saa 12:30 usiku unatazamiwa kuleta upekee kwani timu yoyote itakayoshinda itaongoza ligi ambapo Yanga itafikisha pointi 15 sambamba na Simba ingawa zitatofautiana zaidi kwenye michezo na mabao ya kufunga na kufungwa.

Kwa upande wa Azam ambayo haijapoteza mchezo wowote kati ya mitano iliyocheza, endapo itashinda pia itafikisha pointi 16 na kukwea kileleni jambo ambalo linaongeza msisimko na ushindani mkali kwa miamba hii wakati itakapokuwa inapambana leo.

Mechi hii ni kisasi zaidi kwa Azam kwani mara ya mwisho ilipokutana na Yanga ilikuwa ni Agosti 9, mwaka huu katika Kombe la Ngao ya Jamii hatua ya nusu fainali na kupoteza mabao 2-0, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga.

Kama haitoshi katika Ligi Kuu Bara mara ya mwisho zilipokutana Azam ilipoteza pia mabao 3-2, mechi iliyochezwa Desemba 25 mwaka jana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa mabao yaliyofungwa na Fiston Mayele, Stephane Aziz KI na Farid Mussa.

Mabao mawili ya Azam katika mchezo huo yalifungwa yote na kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Abdul Suleiman 'Sopu' dakika ya 27 na 47.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live