Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga vs Azam, fainali ya kisasi na heshima

Yanga Azam FC 000 Yanga vs Azam

Sun, 11 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Timu mbili zilizotinga fainali ya Ngao ya Jamii kitemi, Yanga na Azam leo zitatoa majibu ya ipi ilikuwa na maandalizi bora ya msimu mpya wakati zitakapokutana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 1:00 usiku zikitanguliwa na mechi ya kuwania mshindi wa tatu kati ya Simba na Coastal Union itakayoanza uwanjani hapo saa 10:00 jioni.

Yanga iliingia fainali baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba katika mechi ya nusu fainali iliyochezwa katika Uwanja huohuo wa Benjamin Mkapa, Agosti 8 wakati Azam FC iliichapa Coastal Union kwa mabao 5-2 katika nusu fainali nyingine iliyofanyika katika Uwanja wa New Amaan Complex siku hiyohiyo.

Mchezo huo wa fainali leo utachezeshwa na refa Ahmed Arajiga kutoka Manyara ambaye atasaidiwa na Frank Komba wa Dar es Salaam na Mohammed Mkono wa Tanga huku Amina Kyando wa Morogoro.

Huo ni muendelezo wa Arajiga kuichezesha Azam FC kwenye Ngao ya Jamii baada ya kusimama katikati katika mechi iliyopita ya nusu fainali ambayo Azam FC iliibuka na ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.

Mkono yeye alikuwa refa msaidizi katika mchezo wa nusu fainali nyingine ya mashindano hayo ambao Simba ilifungwa bao 1-0 na Yanga.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pia imempanga Soud Abdi kuwa mtathmini wa waamuzi katika mechi hiyo.

Ubora ambao kila moja imekuwa nao kwenye safu ya kiungo, umekuwa silaha muhimu kwa Azam na Yanga kupata matokeo mazuri katika mechi tofauti ambazo timu hizo zimekuwa zikicheza.

Lakini pia timu hizo kila moja inajivunia kuwa na kipa wa daraja la juu na hivyo kuwa na uhakika wa ulinzi imara wa lango ambapo Yanga itamtegemea Djigui Diarra.

Namba zinaongea

Yanga imekuwa na historia nzuri ya ubabe dhidi ya Azam FC na hilo linajidhihirisha katika michezo mitano ya mashindano tofauti ambayo timu hizo zimecheza siku za hivi karibuni. Katika mechi hizo tano zilizopita baina ya timu hizo, Yanga imeibuka na ushindi

mara nne na Azam FC imepata ushindi mara moja tu. Mchezo mmoja kati ya minne ambayo Yanga ilipata ushindi, uliamriwa kwa mikwaju ya penalti baada ya timu hizo kumaliza dakika 120 zikiwa na matokeo ya sare tasa na mechi nyingine tatu, ilipata ushindi wa ndani ya dakika 90 kama ilivyo kwa ushindi wa mechi moja ambao Azam iliupata.

Yanga ina wastani mzuri wa ufungaji wa mabao katika mechi hizo kwani imepachika idadi ya mabao saba ikiwa ni wastani wa bao 1.4 wakati Azam FC yenyewe imefunga mabao manne tu ikiwa ni wastani wa bao 0.8.

Uwezo wa kufumania nyavu ambao umeonyeshwa na timu hizo katika mechi mfululizo ambazo zimecheza hivi karibuni unalazimisha makipa na mabeki wa kila upande kuhakikisha wanafanya kazi ya ziada ili kuhakikisha milango ya timu zao inakuwa salama katika mechi hiyo.

Katika mechi tano mfululizo zilizopita, Azam FC imefunga idadi ya mabao 10 ikiwa ni wastani wa mabao mawili kwa kila mchezo na ni mara moja tu kati ya mechi hizo tano, ambapo ilimaliza bila kufunga bao lolote.

Yanga kwenye michezo mitano mfululizo iliyopita, imefumania nyavu mara tisa ikiwa ni wastani wa bao 1.8 kwa mechi.

Pambano la mafahari wawili

Kulikuwa na ushindani mkubwa msimu uliopita baina ya Stephane Aziz Ki na Feisal Salum 'Fei Toto' ambao mwishoni Aziz Ki aliibuka mshindi. Nyota huyo wa Yanga kutoka Burkina Faso alimuacha kwenye mataa Fei Toto kwa kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu na kisha kuibuka mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa Ligi kisha kuchukua tuzo ya kiungo bora wa ligi. Ushindani wao unaonekana unarudi upya msimu huu kutokana na kile ambacho wamekifanya kwenye mechi za hivi karibuni za timu zao.

Fei Toto amefunga mabao matatu katika mechi sita zilizopita za Azam FC kama ilivyo kwa Aziz Ki ambaye amefunga idadi hiyo ya mabao kwa Yanga katika mechi tano zilizopita.

Gamondi, Ferry imani juu

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema wanapaswa kuongeza umakini katika mchezo huo ingawa wana matumaini ya kuwa mabingwa.

“Huu ni mchezo wa fainali, unapaswa kuwa makini sana. Nakumbuka vyema mchezo uliopita pale Zanzibar (dhidi ya Azam). Tayari tunayo picha sahihi tunapaswa kwenda na mbinu gani dhidi ya Azam FC. Niwahakikishie Yanga ni timu imara sana, ukitazama mchezo uliopita, Simba walitengeneza nafasi moja tu kwa sababu tulikuwa imara kwenye kila idara,” alisema Gamondi. Kocha wa Azam FC, Bruno Ferry amesema kuwa wana kikosi kizuri ambacho kipo tayari kwa mechi hiyo ya kesho.

“Hatuna presha. Mwanzoni watu waliamini changamoto ni kubwa sana kwa Azam FC lakini sasa wana imani kubwa na kile tunachokifanya. Naamini mechi itakuwa ngumu na ya wazi kwa vile zinakutana timu mbili ambazo zinacheza soka zuri,” alisema Ferry.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live