Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga vinara mashuti kulenga lango 2023/24

Aziz KI XJKT TZ.jpeg Yanga vinara mashuti kulenga lango 2023/24

Tue, 4 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Yanga na Azam wakikiwasha Zanzibar kwenye mechi ya fainali ya Kombe la FA juzi na Yanga kuibuka mabingwa kwa mikwaju ya penati katika Uwanja wa New Amaan Complex, timu hizo zimeweka rekodi tofauti katika Ligi Kuu mapema wiki iliyopita.

Yanga imeweka rekodi ya kuwa kinara wa kupiga mashuti mengi yaliyolenga lango, huku Azam FC waking'ara kwa kupiga mashuti yaliyotoka nje.

Kwa mujibu wa dawati letu la takwimu za michezo, na chanzo kingine ndani ya Bodi ya Ligi, Yanga imepiga mashuti 205 ambayo yamelenga lango, ikiwa ndiyo timu iliyoongoza kufanya hivyo, ikifuatiwa na Azam FC, ambayo mashuti yake 196 yalilenga, huku Simba ikishika nafasi ya tatu, yenyewe ikitandika mashuti 177 yaliyoenda kwenye usawa na lango.

Tabora United, ndiyo iliyopiga mashuti machache yaliyolenga, ikifanya hivyo mara 93 tu, ikifuatiwa na Coastal Union mara 96, na Geita Gold ikipiga mara 99.

Kwa mashuti ambayo yalikwenda nje, Azam FC ndiyo kinara wao, ikifanya hivyo mara 220, ikifuatiwa na Mtibwa Sugar iliyopiga mashuti fyongo mara 209, Yanga ya tatu ilipiga makombora 192, huku Mashujaa FC ikipiga mashuti machache zaidi yaliyotoka nje, ikifanya hiyo mara 125.

Takwimu zinaendelea kuonyesha mabeki wa Coastal Union ndiyo waliookoa hatari nyingi zaidi langoni mwao msimu huu, ikifanya hivyo mara 334, Mashujaa FC na Prisons zikiondoa hatari langoni mwao mara 321.

Mabeki wa Yanga wameokoa hatari machache zaidi katika ligi hiyo iliyomalizika, wakifanya hivyo mara 157, wakifuatiwa na wa Simba wakiokoa mara 177.

Ihefu FC, kwa mujibu wa takwimu zetu na vyanzo kutoka Bodi ya Ligi, ndiyo timu ambayo viungo wao wa kati walizuia hatari nyingi kuelekea langoni mwao.

Waliharibu mpango ya wapinzani na kunasa mipira mara 491, wakifuatiwa na Prisons mara 445, KMC mara 441, huku viungo wa JKT Tanzania wakishika nafasi ya mwisho kwa kunasa mipira ya wapinzani, wakifanya hivyo mara 331, wakifuatiwa na Tabora United, mara 333.

Hata hivyo Mtibwa Sugar na Geita Gold zimeshuka daraja moja kwa moja wakati Tabora United na JKT Tanzania zitatakiwa kupambana kujinusuru kwa kujaribu tena bahati kwa kucheza michezo ya mtoano.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live