Yanga wanaanza Ligi. Ni safari mpya ya kulisaka gwaride lingine zito la mwisho wa msimu. Wanaanza na KMC katika mechi ambayo kiufundi itakuwa na gongagonga nyingi na burudani ya aina yake kutokana na staili ya uchezaji ya Yanga mpya ya Miguel Gamondi.
Yanga ambayo imeonyesha mpira wa kasi kwenye mechi tatu zilizopita, imekuwa maridadi pia katika gongagonga na kushambulia kupitia pembeni. Lakini KMC mpya ya Abdihamid Moallin imekuwa ikicheza soka la kuvutia na ina mabadiliko makubwa ya kiuchezaji ikianza na mechi iliyopita dhidi ya Namungo ugenini ilikolazimisha sare.
Yanga ambao ni mabingwa wa ligi mara 29, inaingia katika mchezo huu ikiwa na rekodi ya kulichukua taji hilo mara mbili mfululizo, huku mashabiki wake tangu juzi kwenye mitandao ya kijamii ya klabu hiyo wakikomenti kwa wingi wakimshinikiza Gamondi kumwanzisha Straika Mghana, Hafiz Konkoni ili wajue kama yaliyomo yamo tofauti na sasa anavyomchezesha dakika zisizozidi 10.
Timu hizi zinakutana huku zote zikiwa na makocha wapya na Yanga inaongozwa na Muargentina, Gamondi aliyechukua nafasi ya Nabi huku kwa KMC ikiongozwa na kocha wa zamani wa Azam FC, Moallin.