Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga shughuli imeisha

Yanga 8 Sehemu ya kikosi cha Yanga

Fri, 7 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga imeingia kambini kuanza kazi kibabe na jana ilikuwa na dozi mara mbili ikijipanga tayari kupambana na Waarabu wa Sudan, Al Hilal huku kocha Nasreddine Nabi akarusha kombora zito angani na kufichua Kwa Mkapa anaingia na busta tupu kumaliza kazi mapema nyumbani.

Yanga inatarajiwa kuwa wenyeji wa Al Hilal katika mechi ya mkondo wa kwanza ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kurudiana nayo wiki ijayo baadaye nchini Sudan na Nabi alisema kurejea kwa mastaa wake waliokuwa majeruhi kumempa jeuri mapema.

Akizungumza Kocha Nabi aliyeiongoza Yanga kwenye mechi 42 za Ligi Kuu Bara bila kupoteza tangu Aprili mwaka jana, alisema anafahamu mchezo huo utakuwa mgumu akikutana na timu yake ya zamani, ila hata wao Al Hilal wanafahamu wanakwenda kukutana na timu ngumu.

Nabi alisema anafuatilia taarifa mbalimbali za Sudan zikimzungumzia yeye na hata timu hiyo, lakini akafichua nao pia wanahofia rekodi ya Yanga katika miaka hii miwili.

“Nimeishi pale wananifahamu na wanasema mengi kuhusu Yanga, lakini kikubwa hata wao wanajua kwamba wanakwenda kukutana na Yanga tofauti katika kipindi cha miaka miwili,” alisema Nabi na kuongeza;

“Nafahamu itakuwa ni mechi ngumu ndio maana hata wao wameamua kwenda kujipanga sehemu kabla ya kuja hapa, kila timu ina nafasi ya kushinda huu ni mchezo wa soka tunatakiwa kuwa katika ubora mkubwa ili tupate matokeo mazuri hapa nyumbani.”

Kocha huyo alisema amefurahishwa mno kwa kurejea kwa baadhi ya wachezaji wake waliokuwa majeruhi na kuugua akisema hatua hiyo itawaongezea nguvu kwani atawafungia busta Kwa Mkapa ili kumaliza mambo, japo anaendelea kuwafuatilia kwa karibu mastaa wake hao kwenye mazoezi.

“Aucho (Khalid) amerudi ni hatua nzuri kucheza mchezo wa ligi uliopita, Aziz (KI) naye yupo kambini tutamwangalia katika mazoezi juu ya ubora wake, lakini tunaamini atakuwa tayari kwa mchezo huo wa Jumamosi,” alisema Nabi na kuongeza;

“Tunahitaji kuwa kamili kama familia ili tuweze kupata mafanikio ambayo kila mwanachama na mashabiki wetu wanayaombea, hii ni mechi kubwa, kitu kinachonivutia morali kwa wachezaji iko juu sana. Tunatakiwa kuwa imara kwenye ulinzi lakini pia kuwa na makali katika kutengeneza nafasi na kuzitumia, hiki ndio kitu ambacho tunakipigania katika mazoezi sasa, hii sio mechi ambayo utakuwa na hali ya kawaida kama unatengeneza nafasi halafu usizitumie.”

Mara ya mwisho kwa Yanga kucheza makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni 1998, japo mara mbili 2016 na 2018 ilicheza hatua hiyo Kombe la Shirikisho.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live